Twiga Stars yaipiga wiki Mauritania

Muktasari:


Twiga Stars inashiriki mashindano hayo ikiwa timu mwalikwa sambamba na Mauritania baada ya kujitoa kwa timu za Misri na Libya ambazo ni miongoni mwa timu kutoka nchi zinazounda UNAF.

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeanza vyema baada ya kuifunga Mauritania bao 7-0 katika mechi ya ufunguzi ya mashindano ya soka kwa wanawake yanayosimamiwa na Shirikisho la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini (UNAF) yanayofanyika Tunis, Tunisia.

Mechi hiyo imepangwa leo Ijumaa mchana Uwanja wa El Kram uliopo jijini Tunis unaoingiza idadi ya mashabiki 5,000 huku Twiga Stars ikipata ushindi huo dakika 45 za kipoindi cha kwanza na mashindano hayo yanachezwa kwa mtindo wa ligi ambapo timu itakayokuwa na pointi nyingi ndio itakayotwaa taji.

Twiga Stars inashiriki mashindano hayo ikiwa timu mwalikwa sambamba na Mauritania baada ya kujitoa kwa timu za Misri na Libya ambazo ni miongoni mwa timu kutoka nchi zinazounda UNAF.

Mabao ya Twiga yalifungwa na Amina Ally dakika ya 13, Opa Clement dakika 17, Enekia Kasonga dakika ya 27 na 30 na Asha Hamza ambaye ameingia kambani mara mbili dakika ya 23 na 45.

Kipindi cha pili wapinzani walirudi kwa nguvu wakisaka bao la kusawazisha hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika hawakufanikiwa kupata bao hata moja la kufutia machozi zaidi walifanikiwa kuzuia kuongezwa mabao.

Mashindano hayo ya UNAF kwa wanawake  yatamalizika Februari 22 na yanashirikisha jumla ya timu za taifa kutoka mataifa matano ambapo mbali ya Tanzania na Mauritania zilizoalikwa, nyingine ni Tunisia, Algeria na Morocco.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, Tanzania inayatumia mashindano hayo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano matatu makubwa ya soka barani Afrika kwa wanawake ambayo timu zake inashiriki.