Twiga Stars kibaruani leo Tunisia

Friday February 14 2020

Tiwga Stars kibaruani leo Tunisia,TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’,Shirikisho la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini ,

 

By Charles Abel

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ leo Ijumaa saa chache zijazo itakuwa kibaruani dhidi ya Mauritania katika mechi ya ufunguzi ya mashindano ya soka kwa wanawake yanayosimamiwa na Shirikisho la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini (UNAF) yanayofanyika Tunis, Tunisia.

Mechi hiyo imepangwa kuanza mnamo saa 7.00 mchana kwa muda wa Tanzania ambapo itachezwa Uwanja wa El Kram uliopo jijini Tunis unaoingiza idadi ya mashabiki 5,000 na kisha itafuatiwa na mchezo baina ya wenyeji Tunisia na Morocco ambao utachezwa kuanzia saa 9.15 alasiri.

Twiga Stars inashiriki mashindano hayo ikiwa mwalikwa sambamba na Mauritania baada ya kujitoa kwa timu za Misri na Libya ambazo ni miongoni mwa timu kutoka nchi zinazounda UNAF.

Mashindano ya UNAF kwa wanawake ambayo yatamalizika Februari 22 yanashirikisha jumla ya timu za taifa kutoka mataifa matano ambapo mbali ya Tanzania na Mauritania zilizoalikwa, nyingine ni Tunisia, Algeria na Morocco.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wilfred Kidao, Tanzania inayatumia mashindano hayo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano matatu makubwa ya soka barani Afrika kwa wanawake ambayo timu zake inashiriki.

“Ukiangalia kikosi kilivyo, kina mchanganyiko wa wale wakubwa, vijana wenye umri chini ya miaka 20 na pia wale ambao umri wao uko chini ya miaka 17. Tumefanya hivyo kwa sababu muda unatubana hivyo hizo timu zinapaswa kujiandaa mapema na pamoja.

"Timu yetu ya wakubwa inajiandaa na mashindano ya kufuzu AWCON ambayo tumepangwa kucheza dhidi ya Kenya, tuna mechi dhidi ya Uganda kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia na timu yetu ya U20 pia ina mechi dhidi ya Senegal. Nia na mkakati wetu ni kushiriki fainali hizo zote ndio maana tunapambana kuhakikisha tunaziandaa vizuri hizo timu,” alisema Kidao.

Jumla ya wachezaji 20 wapo na Twiga Stars nchini Tunisia huku kundi kubwa likiwa ni wale wenye umri wa chini ya miaka 20 na pia wale wa umri chini ya miaka 17 huku kukiwa na wachache wanaouvuka umri huo.

Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji,  Tausi Abdallah (Yanga), Anastazia Katunzi (JKT Queens), Enekia Kasonga (Alliance Queens), Juliet Singano (Simba Queens), Happy Hezron(Yanga Princess), Fatuma Issah (Simba Queens), Fatuma Hassan (Yanga Princess), Amina Ally (Yanga Princess), Diana Lucas (Ruvuma Queens) na Asha Rashid (JKT Queens).

Wengine ni Mwanahamisi Omary (Simba Queens), Phiromena Daniel (Mlandizi Queens), Opa Daniel (Simba Queens), Violeth Machela (Simba Queens), Fatuma Hatibu (JKT Queens), Asha Hamza (Kigoma Queens), Eva Jackson (Kigoma Queens), Zubeda Mgunda (Simba Queens), Ester Mabanza (Alliance Queens) na Aisha Masaka (Alliance Queens).

Advertisement