JAMVI LA KISPOTI : Tunataka mafanikio kwenye soka bila kuwekeza

Friday July 5 2019

 

By Khatimu Naheka

Taifa Stars wanatua nchini leo wakitokea Misri walikokuwa wakishiriki Fainali za Mataifa Afrika.

Stars inarejea kichwa chini na sina wasiwasi ukifika katika mapokezi yao pale leo kila mchezaji atachagua njia yake kutokana na aibu.

Shida sio wachezaji wamefanya vibaya lakini vichwa vyao vitakuwa vinauma kutokana na walichokutana nacho Misri kimewashangaza.

Walichokutana nacho Stars ni sawa uwe mpiganaji ngumi alafu ukakutana na mtu anayejua kuzichapa zaidi yako na akakuchapa kisawasawa.

Stars kupoteza mechi zake tatu ni matokeo ya haki kutokana na aina ya timu walizokutana nazo hakuna waliobahatisha katika safari hiyo.

Pengine ni Stars ambao walifika hapo bila mpango wa muda mrefu kutokana na maisha yetu.

Advertisement

Mataifa mengi ambayo yamepeleka timu zao Afcon yamewekeza kwa nguvu ya kutosha katika kufikia mafanikio hayo wanayoogelea sasa.

Pengine wanaweza kuw Stars tu ambao uwekezaji uliofanywa na serikali ukawa kulipia gharama za safari tu na mamno mengine madogomadogo.

Kila timu imekuwa na mkoni mkubwa wa uwezeshaji kutoka katika serikali zao mbalimbali.

Hapa kwetu maisha ni tofauti baada ya serikali kuwekeza jukumu hilo wameachiwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya kila kitu.

Ikitokea nao wakapotea kidogo shida inakuja kwa nchi nzima lakini hatujui tunakosea wapi.

Nimeshangaa kuona wabunge wakishambuliana na baadhi ya wadau hasa kamati ya hamasa lakini anguko la Stars limeanzia bungeni.

Bunge limeshindwa kuwa na mipango ya kusimamia timu za taifa kupitia bajeti ya wizara husika hakuna fedha zinazowekezwa kwa kutafuta mafanikio ambayo tunayalilia.

Unapitisha bajeti ya wizara ambayo inakosa fungu la kugharimia timu za taifa alafu bado unasafiri kwenda Cairo kusubiri Stars ishinde hiki ni kichekesho.

Bado tuna siasa za ajabu katika mambo ya msingi huu ni utawala wa kuambiana ukweli kama ambavyo Rais John Magufuli anavyosema majukwaani nafikiri watendaji wa chini yake wanatakiwa kuacha propaganda na kuuweka ukweli hadharani na sio kumpotosha Rais wa kuchafuana.

Nchi imekwama kimichezo hasa soka,nchi inafedheheka kwa makosa yetu ya kuondoa utaalamu na kupunguza siasa katika mambo ya msingi.

Kama tunataka mafanikio ya kweli basi tujitathimini kwa kina kwamba bado hatujawekeza kiasi cha kutaka mafanikio ambayo tunayalilia sasa.

Kama tunataka mafanikio basi tunapojikwaa tunapajua hakuna tunachozalisha kwa utaratibu basi ni vyema sasa tukaweka nguvu kubwa kupata wachezaji watakaokuwa tayari kucheza timu za taifa ili baadaye tuje na sababu ya msingi kuanza kuwalaumu makocha.

Hatuzalishi wachezaji tunasubiri wajitokeze kama uyoga alafu tunataka kulaumu hii sio sawa ni wakati wa kubadilika.

Advertisement