Tshishimbi: Mashabiki mtusamehe, ni wakati wa kujipanga upya

Muktasari:

Jambo la pili ambalo limeniumiza zaidi ni jinsi gani tumepoteza nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa kwa msimu ujao, huu ni wakati mgumu zaidi ambao klabu inapitia inatufanya sasa kuwa na mwaka wa tatu zaidi kucheza bila mafanikio.

Sina furaha. Itanichukua muda mrefu kuweza kukubaliana na hili ambalo lilitokea Julai 12 pale Uwanja wa Taifa. Kikubwa ni timu yangu kupoteza mchezo kwa idadi kubwa ya mabao katika mchezo ule dhidi ya wapinzani wetu, Simba.

Kinachoniumiza ni jinsi tulivyopoteza mambo mawili makubwa. Kwanza kufungwa kwa idadi kubwa kama ile ya mabao katika maisha yangu ya soka sijawahi kupoteza kwa mabao mengi kama vile hasa mchezo dhidi ya wapinzani wetu wakubwa.

Jambo la pili ambalo limeniumiza zaidi ni jinsi gani tumepoteza nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa kwa msimu ujao, huu ni wakati mgumu zaidi ambao klabu inapitia inatufanya sasa kuwa na mwaka wa tatu zaidi kucheza bila mafanikio.

Acha niseme kitu kuhusu ile mechi wengi wanaweza kuwa hawakukubali kiwango changu, lakini sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana na kile ambacho kocha aliniomba - kucheza ile mechi.

Nilijua kwamba bado sikuwa vizuri sana, lakini kwa hali ambayo tulikuwa nayo ndani nililazimika kumwelewa kocha na kuamua kuingia uwanjani ili niweze kuisaidia klabu - kuitetea katika mchezo muhimu. Mimi ni mwanajeshi kuna wakati unatakiwa kuingia vitani hata kama umeumizwa kwa risasi mguuni.

Mashabiki wetu nafahamu kwamba hamna furaha na kile ambacho kilitokea katika mchezo ule na niseme tu binafsi kwa niaba ya wenzangu nichukue fursa hii kama wewe ni shabiki wa Yanga, nikuombe radhi kwa matokeo yale. Tulifanya makosa makubwa na mchezo wa soka ni mchezo wa makosa. Tulifanya makosa na yalitugharimu, tusameheane na sasa tujitahidi kurudi kuwa wamoja ili safari iendelee.

Safari inayopaswa sasa kuanza hata kama tuna maumivu katika mioyo yetu ni kujipanga na maisha mapya ambapo kwanza tunatakiwa kujifanyia tathimini wapi tumekosea, kipi kifanyike na baada ya hapo kazi inatakiwa kuendelea.

Matokeo ambayo tumeyapata katika mchezo ule yanatuonyesha changamoto mbalimbali ambazo zipo katika kikosi chetu. Mpira ni mchezo unaochezwa sehemu ya wazi kuna kazi ambayo mashabiki na wanachama wanatakiwa kushikamana na uongozi kisha kuhakikisha tunazifanyia kazi changamoto.

Kikosi chetu kimeonyesha ni jinsi gani kinatakiwa kuundwa kwa umakini mkubwa ili kila kitu kirudi katika afya yake ya awali ambayo kama timu inahitajika kuwa nayo. Hili ndilo muhimu kwa sasa.

Nimekuwa nikisisitiza zaidi huko nyuma kwamba kuna kazi ya usajili inatakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa ili timu iache kuleta maumivu kwa wanachama na mashabiki wetu. Inaumiza kuona mashabiki wanakuwa na imani kubwa na timu yao, wanapambana lakini mwisho wa siku timu inashindwa kuwapa kile ambacho wanatarajia.

Huu ni wakati wa kutuliza akili, kamwe tusifanye makosa ya kufanya uamuzi wa papara kisha tukaja kupoteza zaidi ya haya ambayo yametokea sasa na huko nyuma. Umakini mkubwa ndio utatusaidia kutoka hapa pagumu tulipokwama.

Tukimaliza kufanya kazi hiyo, pia nigusie suala la nidhamu. Kuna maisha lazima yahakikishe yanafanyiwa kazi hasa kwa usimamizi mzuri wa nidhamu kwa wachezaji wenzangu. Klabu hii ni kubwa na ifike sehemu lazima mchezaji yeyote hata kama atafunga mabao 200, aiheshimu kwa kadri anavyoweza au anavyotakiwa.

Kuna makosa yanafanyika katika usimamizi wa nidhamu na kama hayatafanyiwa kazi ipo siku yataleta maafa zaidi katika timu. Hili niwaachie viongozi ambao wanatakiwa kulifanyia kazi kwa umakini, naamini kila kitu wamekiona kwenye timu.

Wakati nafika hapa mambo mengi yalikuwa yanasimamiwa kwa umakini mkubwa na hakuna timu itafanikiwa kama hakutakuwa na usimamizi mzuri wa nidhamu kwenye kikosi. Narudia hii ni klabu kubwa ni lazima iheshimiwe siku zote, mchezaji au kocha anapita na klabu inabaki palepale.

Yanga inaweza kurudi katika maisha yake ya awali kama tutatuliza akili na kufanya uamuzi sahihi katika kuchagua maisha ambayo tunatakiwa kuishi.

Kama hili halitafanyika tutazidi kuwaumiza wadau wetu ambao ni mashabiki na wanachama.

Narudia tena kwa kumalizia nafahamu mmeumia sana, tunawaomba radhi kwa usumbufu wote tuliousababisha kwa matokeo yale, na sasa tushikamane kutafuta maisha bora ya kesho na daima huko mbele. Niwakumbushe hili, daima mbele nyuma mwiko. Asanteni.