Tshishimbi: Huu ndio ukweli kuhusu maumivu yangu Yanga

Muktasari:

Leo naomba nizungumzie suala la kukaa kwangu nje kwa muda wa kama wiki tatu au mbili lakini pia nitagusia juu ya uamuzi wangu wa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Simba.

HAKIKA msimu wa 2019-20 unaomalizika baada ya mechi mbili zijazo haukuwa mzuri kwetu kama Yanga. Kulikuwa na milima na mabonde mengi kuliko utulivu.

Najua kwamba mashabiki wanachama, viongozi na hata sisi wenyewe wachezaji hakuna aliyefurahia ambacho kimetokea ndani ya msimu huu. Yapo mengi ambayo tulipanga kama timu yakiwa ni malengo tuliyotaka kuyafikia ndani ya msimu huu lakini karibu yote hatukuyafikia.

Kutokufikia kwetu lazima tukae chini kwa utulivu na kujaribu kufikiri wapi tulikwama kisha tukipata majibu tunapaswa kukaa chini na kutafuta akili mpya ya kipi kifanyike kama timu kuhakikisha tunafuta taswira hii mbaya ndani ya klabu yetu. Sio afya kwa klabu kubwa kama Yanga kukosa kombe lolote ndani ya misimu mitatu. Binafsi nitakuwa na yangu baada ya mchezo wa mwisho na nitawapa hapa wasomaji wangu.

Leo naomba nizungumzie suala la kukaa kwangu nje kwa muda wa kama wiki tatu au mbili lakini pia nitagusia juu ya uamuzi wangu wa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Simba. Sikutaka kuyaongelea haya lakini imenibidi kufanya hivyo ili kuondoa upotoshaji ambao unaendelea katika mitandao na hasa kwa mashabiki wa Yanga na hata kwa viongozi wangu.

Iko hivi. Kwa muda nilikuwa nje ya timu katika ratiba ya kuhakikisha napona vizuri maumivu yangu ya goti na nakumbuka wakati naonana na daktari kwa mara ya kwanza aliniambia kinachonisumbua hakinizuii kucheza lakini ni vyema nikapona vuzuri kabisa ili nikirudi niwe tayari kuisaidia timu yangu.

Kwa wasiofahamu nafasi ambayo nacheza uwanjani ni ngumu inahitaji nguvu kubwa na kupambana sana lakini pia kuna wakati unaweza kuumizwa kwa kugongwa mara kwa mara. Nafikiri msingi wa ushauri wa madaktari ulikuwa hapa sana.

Niliwaelewa na kuamua kukaa nje kwa muda huo huku nikifanya ratiba mbalimbali za mazoezi ya taratibu kwa jinsi ya maelekezo yao kama madaktari. Nafurahi kwamba ratiba hii hata makocha waliipitisha na ilikuwa inakwenda vyema.

Wakati wa kurudi kwangu uwanjani ulifika ikiwa karibu kabisa na ule mchezo dhidi ya Simba na nilipojiunga na timu siku moja ikiwa inatokea Bukoba nilifurahi kuungana na wenzangu na kubwa ilikuwa ni morali kuelekea mchezo ule mgumu.

Wakati namaliza mazoezi ya siku ya kwanza makocha walinifuata na kuniuliza wamefurahi kuona nafanya mazoezi vizuri wakataka kujua kama nasikia maumivu yoyote nikawaambia hapana lakini bado tu mwili haijachangamka kisha wakaniuliza kama nitaweza kucheza mchezo dhidi ya Simba. Kiukweli nilisita kidogo kukubali lakini baadaye niliwaambia naweza kucheza ingawa kwa kumalizia dakika 40 za mwisho.

Uamuzi wangu wa kusema hivyo najua kwamba kama ningeanza ningejiweka katika nafasi mbaya ya kuweza kuumizwa kwa kuwa wenzangu wangekuwa sawa kunishinda mimi lakini baadaye ushauri ukaja kwa hali ya kikosi, kocha aliona bora nipambane nianze. Na mazingira ambayo kocha alinieleza na ukichukulia na kwamba naithamini hii klabu, niliona nisaidie kwani huo ndio uanajeshi, nikakubaliana nalo. Nashukuru nilianza taratibu ingawa baadaye mambo yakawa kama yalivyokwenda.

Nimelazimika kutoa ufafanuzi huu baada ya kusikia kwamba wapo wanaosema kwamba eti kuumia kwangu kulihitaji upasuaji na wengine walienda mbali wakidai nilicheza ili niifungishe timu yangu au wapo pia wanaosema nililazimisha kucheza. Hizi sio kauli za kweli, kila kitu kinajulikana.

Watu wanatakiwa kutambua mimi sio mchezaji wa aina hiyo. Najua kuheshimu ofisi yangu na waajiri wangu.

Ndio maana licha ya matatizo yote na vipindi vigumu tulivyopitia kama klabu sijawahi kugoma kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanya.

Ningekuwa mchezaji wa namna hiyo ningesema hata nisicheze kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanya wakidai mikataba mipya lakini nimekuwa mvumilivu katika hii klabu nafikiri ni wakati kwa mashabiki baadhi kuheshimu mchezaji ambaye amewaheshimu kwa kiasi ambacho nimefanya.

Nimeona nieleze hili kwa kuwa mpira ni kazi yangu na kilichonitisha zaidi wapo hata baadhi ya viongozi nao wameshtuka kusikia nina jeraha linalohutaji upasuaji hii sio kweli nilikuwa na maumivu ambayo yalihitaji kupumzika na kama hakuna anayeamini nafikiri ni suala la muda, kama kuna kitu kinataka kufanyika basi ningeomba kisitafutiwe sababu kama ambavyo hili linataka kutumika kusukuma uamuzi.

Tukutane Alhamisi ijayo.