Simba Arusha wamepania kinoma

MRATIBU WA Simba mkoani hapa, Abbas Suleiman Ally alisema wana maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanachukua taji la Ngao ya Jamii leo ingawa wanakiri Namungo ni ngumu.
“Tulianza maandalizi mapema ya mchezo huu na pia mechi za kujipima ambapo tulianza na ile siku ya Simba Day na juzi kucheza na KMC michezo ambayo imetoa taswira ya nini tunapaswa kufanya katika mchezo huu,” alisema
“Namungo sio wageni kwetu kwani tumeshakutana nao msimu huu mara tatu na tumewafunga mara mbili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu mmoja hivyo kwa heshima hiyo hiyo tutaingia siku hiyo uwanjani kuhakikisha tunawashinda,” aliongeza.
Kwa upande wa viingilio, Shirikisho la Soka nchini kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Boniphace Wambura alisema tiketi na kila kitu kinakwenda sawa.
Wambura pia amesema kuwa wameepuka kuweka vipengele vingi vya tiketi za viingilio ili iwe rahisi kukabiliana na walanguzi wanaojipatia fedha bure huku wakiwasumbua mashabiki wanaotaka kuona burudani.
Kamati ya waamuzi imesema waamuzi sita watasimamia mchezo huo akiwemo mwamuzi wa kati Ramadhani Kayoko kutoka jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Soud Abdi alisema kuwa kwa upande wa waamuzi wa pembeni watakuwepo Komba Frank kutoka Dar na Mohammed Mkono (Tanga).