Shime aunguruma Tunisia

Muktasari:

Kocha, Bakari Shime, ametamba kuwachapa wapinzani wao Mauritania katika mchezo wa ufunguzi kwenye mashindano ya UNAF yanayofanyika Tunisia leo Ijumaa.

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Bakari Shime 'Mchawi Mweusi', ametamba kufanya vizuri katika michuano UNAF  (Umoja wa nchi za Afrika) ambapo leo Ijumaa mchana watafungua dimba dhidi ya Mauritania.
Shime na kikosi chake waliondoka nchini majuzi na kuwasili Tunisia juzi Jumatano ambapo jana Alhamisi walifanya mazoezi tayari kwa mchezo huo wa leo.
"Tumejiandaa vizuri kuona tunaifunga Mauritania. Kwetu ni mashindano mazuri kwa sababu yanatoa fursa kwa wachezaji wetu kujiandaa vizuri kutokana na kupata mechi nyingi za majaribio,"alisema Shime.
Alisema, analipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupambana na kupata nafasi za kushiriki mashindano kama hayo kwa maandalizi yaliyo bora.
Timu tano zinazoshiriki mashindano hayo, mbali na Tanzania ni wenyeji Tunisia, Morocco, Algeria na Mauritania.
Tanzania ni timu alikwa kwenye mashindano hayo ya vikosi vya wakubwa wanawake.