Samatta hali tete England

Saturday June 27 2020
SAMATTA PIC

HALI si shwari kwa nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta baada ya chama lake la Aston Villa kupasuka nyumbani jioni hii kwenye mchezo pekee wa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa kunyooshwa bao 1-0 na Wolves na kuzidi kujiweka pabaya kwenye janga la kushuka daraja.
Villa wakiwa kwenye Uwanja wao wa Villa Park, mjini Birmingham walikuwa wakisaka pointi tatu za kuwatoa nafasi ya 19 na kuweka hai matumaini ya kusalia kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao.
Hata hivyo, bao pekee la kipindi cha pili lililowekwa kimiani na Leander Dendoncker katika dakika ya 62 lilitosha kuiweka pabaya Villa iliyomsajili Samatta kutoka Genk KRC ya Ubelgiji.
Villa waliwabana wapinzani wao hao ambao ushindi huo umewafanya wapande kwa nafasi moja katika msimamo kwa kushika nafsi ya tano wakiishusha Man United na kwenda nao maopumziko wakiwa nguvu sawa.
Hata hivyo kipindi cha pili mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Nuno Espirito Santo  kwa kumuingiza Adama Traore akichukua nafasi ya Diogo Jota katika dakika ya 60 ilichangamsha safu ya ushambuliaji wa Wolves na kusaidia kutengeneza bao hilo lililowazamisha kina Samatta.
Villa wamesaliwa na mechi sita zikiwamo tatu dhidi ya vigogo, Man United, Arsenal na Liverpool waliokwishakutwaa ubingwa bila hata kushuka uwanjani baada ya kurahisishiwa kazi na Chelsea.
Chelsea iliifumua Man City juzi usiku na kuwavua taji walililokuwa wakilishikilia kwa misimu miwili mfululizo na kuwapa nafasio Liverpool kuandika historia ya kutwaa taji la Ligi baada ya kulisotea kwa miaka 30. Hilo ni taji la kwanza kwa mabingwa hao wapya wa England katika Ligi Kuu tangu mfumo ulivyobadilishwa mwaka 1992, ikiwa ni miaka miwili tu tangu walipotwaa ubingwa wao wa mwisho mwaka 1990 wakati EPL ikifahamika kama Ligi Daraja la Kwanza.

Advertisement