Rio amtaka Kane atimke zake Spurs

LONDON, ENGLAND. BEKI mwingereza, aliyewahi kukipiga West Ham, Leeds United na Manchester United, Rio Ferdinand amemwambia straika namba moja wa Tottenham Hotspur, Harry Kane kwamba umefika wakati wa kuachana na timu hiyo ili kuhamia kwenye klabu kubwa.
Straika, Kane aliisaidia Spurs kucheza fainali yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na kuchapwa na Liverpool, huku mwaka jana aliisaidia England kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia huko Russia.
Jumatano iliyopita alifunga kwa mkwaju wa penalti wakati Spurs ilipopata sare ya 2-2 dhidi ya Olympiakos kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Ferdinand anaamini kwamba ni wakati wa mshambuliaji huyo kuhamia kwenye timu kubwa inayoendana na hadhi yake.
Ferdinand anachojaribu kusema ni kwamba soka ni mchezo wenye mazingaumbwe, kwamba unaweza ukawa majeruhi kwa msimu mzima, au ukaporomoka kiwango, hivyo unahitaji kutumia wakati wako vizuri ikiwamo kucheza kwenye timu ambayo itakusaidia kushinda mataji.
"Ukiwa na kawaida ya kujifikiria mwenyewe, kama vile Harry Kane, basi anapaswa kuondoka. Kwa sababu ni jambo la kweli, huwezi ukawa kwenye ubora huo huo kila wakati. Unaweza kuwa majeruhi msimu unaofuata, unaweza kushuka kiwango na mambo kama hayo. Huku ukifahamu wazi unahitaji kushinda kitu fulani," alisema Ferdinand.
Beki huyo wa kati aliyewahi kutamba sana kwenye kikosi cha England alisema anamwelewa vyema kiungo Christian Eriksen kwa uamuzi wake wa kutaka kuondoka kwenye timu hiyo kwa sasa kwa sababu anahitaji kwenda mahali patakapomfanya ashinde kitu kabla ya umri na soka kumpa kisogo.