Ozil afichua siri ya kuikosa Olympiacos

Sunday February 23 2020

Ozil afichua siri ya kuikosa Olympiacos,STAA wa Arsenal, Mesut Ozil , Europa League ,

 

LONDON, ENGLAND . STAA wa Arsenal, Mesut Ozil amewatumia ujumbe wa pongezi wachezaji wenzake baada ya kuwachapa Olympiakos kwenye Europa League Alhamisi iliyopita.
Fundi huyo wa mpira hakucheza mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya 32 kwa sababu mkewe mrembo Amine Gulse alikuwa akijifungua.
Ozil alitumia ukurasa wake wa Twitter juzi Ijumaa, siku moja baada ya Arsenal kushinda 1-0, aliandika: "Hongera vijana wangu! Hatua ya kwanza muhimu - hainna kupoteza 2020."
Straika Alexandre Lacazette ndiye mfungaji wa bao pekee kwenye mchezo huo alipomalizia pasi safi kabisa ya kinda Bukayo Saka katika mchezo huo uliofanyika Athens, Ugiriki.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alizungumza mechi hiyo na kusmea: "Ni matokeo mazuri sana. Kwanza tumeshinda ugenini kwenye michuano ya Ulaya, lakini pia kupata ushindi kwenye uwanja wa aina hii, hizo ni pongezi kubwa kwa vijana.
"Tulipata shida kwenye dakika 10 za mwanzo, tulikuwa tunapoteza mipira sana, lakini kwenye kipindi cha pili, ukiweka kando ile mipira ya adhabu, tuliweza kuumiliki mchezo."
Arsenal watashuka uwanjani leo Jumapili kukipiga na Everton kwenye Ligi Kuu England na haifahamiki kama Ozil atakuwa kwenye hali nzuri kucheza mchezo huo utakaopigwa Emirates. Ozil alifunga ndoa na Miss Uturuki, mrembo Amine mwaka jana.

Advertisement