Mziki wa Mnyarwanda wamuibuka Mzee Kilomoni

Muktasari:

  • Niyonzima alionekana kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kipindi cha kwanza kumalizika timu hizo zikiwa sare ya bao moja ambapo Niyonzima aliingia kipindi cha pili.

MZEE Kilomoni ameshindwa kujizuia huko. Ndio, si mnamkumbuka mwasisi na nyota na kiongozi wa zamani Simba, Hamis Kilomoni alikuwa kimya sana hasa tangu alipotangazwa kuvuliwa uanachama, juzi ameibuka buana baada ya kukoshwa na soka tamu ya Haruna Niyonzima lililosaidia kuivusha Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ipo hivi. Siku moja baada ya Simba kufuzu hatua ya robo fainali, Kilomoni ameibuka na kutamka kuwa Haruna Niyonzima muda tu ndiyo ulikuwa unasubiriwa.

Awali Niyonzima ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu kiwango chake kilionekana kuporomoka na hivyo kuwa na shaka ndani ya kikosi hicho.

Katika mechi ya juzi Jumamosi kiungo huyo Mnyarwanda aliingia akitokea benchi akichukua nafasi ya Emmanuel Okwi aliubadilisha mchezo na Simba ilishinda bao 2-1 dhidi ya AS Vita ya DR Congo.

Niyonzima alionekana kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kipindi cha kwanza kumalizika timu hizo zikiwa sare ya bao moja ambapo Niyonzima aliingia kipindi cha pili.

Kilomoni aliyezushiwa kifo juzi, alisema Simba ina uwezo wa kuvuka hata hatua hiyo na kutinga nusu fainali kama tu wachezaji na viongozi pamoja na wanachama wataendelea kuungana na kuleta umoja kama mechi zilizopita.

“Kwanza watu watambue mimi ni mzima wa afya ingawa nasumbuliwa na miguu tu na si vinginevyo, waliosambaza kuwa nimekufa sijui wamepata wapi taarifa hizi.

“Kwakweli kikosi chetu ni kizuri na kimejitahidi kupambana, huo ndio mpira tunaoutaka wanachama na mashabiki wa Simba hata nafasi ya nusu fainali tunayo.

“Niliutazama mchezo wote na kugundua Niyonzima ana kitu cha pekee japokuwa huko nyuma alijichanganya, ila naamini ametambua wapi alijikwaa na kurekebisha makosa yake na hiyo ndiyo nidhamu ya mchezaji maana mpira ni mazoezi na utimamu wa mwili.

“Kikubwa wasiingize starehe kwani wako kwenye vita kali ya kuwapa furaha Watanzania na kuiingizia klabu mamilioni ya fedha, “ alisema Kilomoni

Kuhusu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Kilomoni alisema: “Nafasi ni kubwa ubingwa kubaki Msimbazi, naamini hivyo. Sisi wazee tumewaachia vijana wafanye kazi na tunawaona wanavyofanya ingawa kuna mambo yaliingilia hapo kati upande wa viongozi ila naona wamekaa sawa kwa maslahi ya klabu.

“Kikubwa kocha afanyie kazi safu ya ushambuliaji maana inashindwa kumalizia mipira mingi inagonga mwamba, hilo ni tatizo, ila umoja wao ndiyo utawafanya watetee ubingwa wa ligi, hao Yanga bado nafasi yao ni finyu,” alisema.