Zahera aingia na mfumo 4-5-1, Sadney apewa mikoba kuiua Pyramids

Muktasari:

Ni mechi inayoonekana kuwa na presha kubwa kwa timu zote mbili lakini pamoja na hilo, kila upande umejinasibu kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo ambao umeonekana kuteka hisia za wadau wa mpira wa miguu nchini.

Dar es Salaam.Mshambuliaji Sadney Urikhob ataiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga leo katika kuhakikisha inashinda dhidi ya Pyramids katika mchezo wa mtoano wa kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Urikhob amefunga mabao mawili tu katika mashindano yote tangu alipojiunga Yanga msimu huu hivyo leo atakuwa na jukumu moja la kuthibisha ubora wake mbele ya mashabiki wa Yanga.

Urikhob alifunga bao lake la kwanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zesco jijini Ndola pia alifunga dhidi ya Mbao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo Mnamibia huyo anakwenda katika mchezo afya yake bado ikiwa ni changamoto baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Mbao pia Alhamis alishindwa kumaliza mazoezi na wenzake kutokana na maumivu hayo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameingia katika mchezo huo na mfumo wa 4-5-1 akiwa anajilinda zaidi, na kushambulia kwa shtukiza akitegemea kasi za wachezaji wa pembeni kuanzisha mashambulizi.

Zahera alisema Waarabu wote wanacheza soka la aina moja hivyo, katika mhezo wa leo hawatamsumbua.

“Timu za Afrika Kaskazini, Morocco, Algeria, Misri na hata Tunisia, mchezo wao ni wa aina moja wa kucheza pembeni kwa kushambulia wakitumia viungo wenye kasi. Bahati nzuri nawajua kwani nikiwa kocha wa timu ya Taifa ya DR Congo nimekutana nao, sina shaka nao, najua jinsi ya kuwamudu,” alisema Zahera.

Katika kikosi hicho Urikhob atakuwa mshambuliaji pekee mbele katika nafasi ya kiungo watakuwa watano nahodha Pappy Tshishimbi, Feisal Salum, Makame Abdullaziz, Mapinduzi Balama na Mrisho Ngassa.

Safu ya ulinzi itakuwa chini ya Kelvin Yondani, Ali Ali, Ally Mtoni ‘Sonso’ na Juma Abdul.

Adhabu ya kutumikia kadi nyekundu ya beki Lamine Moro aliyoipata katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Zesco ya Zambia kumempa nafasi Ally kucheza sambamba na Yondani.

Kipa Farouk Shikalo leo ataichezea Yanga kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kimataifa tangu alipojiunga akitokea Bandari FC ya Kenya.

Katika benchi Yanga imeanza na wachezaji saba wanaokizi kikanuni wakiwemo makipa wawili Ramadhan Kabwili na Metacha Mnata ambapo mratibu wa timu hiyo Hafidh Salehe amesema uamuzi huo unatokana na kutaka kukamilisha idadi ya wachezaji wanaohitajika kuwa benchi kutokana na kikosi chao kukabiliwa na majeruhi wengi huku wengine wakikosa vibali.

Wengine ni pamoja na viungo Deuse Kaseke, Patrick Sibomana na Jafary Mohamed, beki Mharami Issa 'Marcelo' huku mshambuliaji akiwa mmoja pekee Juma Balinya.

Uimara wa Yanga ambao unaweza kuwabeba katika mchezo wao leo dhidi ya Pyramids ni kasi ya wachezaji wake wa safu ya ushambuliaji Mrisho Ngassa, Papy Sibomana, Juma Balinya na Sadney Urikhobi.

Kasi hiyo imekuwa ikitumiwa na Yanga pindi inapopokonya mpira kutoka kwa wapinzani au pale inapoanzisha shambulizi, kupiga pasi ndefu ambazo hutumiwa vyema katika kutengeneza nafasi, kufunga mabao au kusababisha faulo.