Tabasamu la Manara, huzuni kwa Miraji Athumani

Wednesday November 13 2019

Mwanaspoti-Tabasamu-la-Manara-Tanzania-huzuni-Miraji-Athumani-Simbasc-Yanga-TFF-Ligi-Kuu

 

By Nicasius Agwanda

Ndugu yangu mmoja asiyekuwa shabiki wa michezo kupindukia alikuja na swali kwangu ambalo lilinipa msukumo wa kushika kalamu na kuandika, kujiuliza na kutafakari kwa kina. Swali lake la msingi lilikuwa linahusiana na wingi wa mashabiki ndani ya viwanja hususani mechi za klabu kubwa Simba na Yanga.
Akiwa mtulivu kabisa alinitupia swali kuwa, kipi kinachangia wingi wa mashabiki uwanjani, Haji Manara au Meddie Kagere, Antonio Nugaz au Balinya na Molinga? Kwa sababu inawezekana nimewahi kuwa mmoja kati ya watu ambao wanaamini soka ndilo linalopeleka watu uwanjani, nikajibu ni Mkude, Bocco, Kagere, Chama na akina Molinga, Sadney na Kelvin Yondan.
Akiwa anatikisa kichwa akaniuliza tena, nani anapeleka mashabiki uwanjani pale Old Trafford, Anfield, Camp Nou, Santiago Bernabeu na Emirates? Haraka nikaorodhesha majina ya Rashford, Mane, Messi, Hazard na Aubameyang. Swali lililonipelekea kuelewa haswa nini alikuwa anataka likafuata na kupenya barabara kwenye ngoma za masikio yangu ambazo zilikuwa zimekosa mirindimo sahihi katika swali la awali.
Ni nani huwa anahamasisha twende tukaone anachofanya Messi au Ronaldo ndani ya uwanja? Jibu likaja kichwani haraka tu kuwa ni hakuna bali chapa zao zimetengenezwa na zinauzika vyema kabisa na wana mashabiki ambao wanaamini hawa wanawakilisha nembo ya klabu wanazoshabikia.
Inawezekana hili likajibu maswali mengi ambayo yalikosa majibu kwanini wakati mwingine inatumika nguvu kubwa zaidi kuhakikisha watu wanajaa viwanjani. Lilikuwa swali la msingi ambalo lilinifanya kujaribu kukumbuka kila chembe ya uendeshaji wa soka letu.
Inawezekana hii ikawa ni dhambi ambayo tumeendelea kuifanya na inadumu kwa muda sasa na tumeikumbatia kwa sababu tunaipenda, inatufurahisha na inatupa msisimko wa soka letu. Vyombo vya habari vinajaa kwa Haji Manara kuliko kwa Chama aliyefunga goli zuri la kisigino, zinajaa kwa Nugaz kuliko Sibomana anayefunga kwa mpira wa adhabu au kuliko Metacha anayeokoa mikwaju ya penalti inayowapeleka Yanga hatua inayofuata kwenye michuano ya kimataifa.
Kwa sababu gani? Manara ataizodoa Yanga na kutoa lugha ambayo itazungumzika mitandaoni kisha Nugaz au Bumbuli watajibu mapigo kwa maneno ambayo yatawaridhisha mashabiki wao kuwa wamejibu mapigo.
Mashabiki wa Yanga hawaumii kwa sababu timu yao haijasajili vyema bali wanalia kwa sababu wataweka wapi sura zao Haji Manara akianza kuzungumza. Kama haitoshi, kuelekea michezo mbalimbali ambayo klabu zetu zinacheza, sio wachezaji wala makocha wanaozungumzia hali ya klabu, wachezaji na mbinu bali ni wasemaji ndio wanaosimama kidete kuelezea mipango na matarajio ya mechi husika. Tunatembea kinyume na dunia inavyoenda, inawezekana ikawa sio mbaya kwa sababu wataalamu wa mambo wanaamini ukipindua meza na kufanikiwa basi wewe ni shujaa lakini mfumo wetu haupo sawa. Haupo sawa kwa sababu imefika hatua mwandishi wa habari ni staa kuliko mchezaji na anaheshimika mtaani kuliko mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao katika Ligi Kuu.
Wachezaji wetu majina yao yanabeba maana wanapokuwa ndani ya uwanja lakini yanapoteza mvuto wanapovua jezi na kutoka nje ya uwanja. Ndio maana leo hii Haji Manara ana mvuto wa matangazo kuliko Kagere, Shaffih Dauda anavutia kibiashara kuliko Kelvin Yondani na Edo Kumwembe anabeba uhalisia wa soka kuliko Salum Abubakar.
Ni rahisi kumsikiliza Manara na kumuelewa kuliko Patrick Aussems, ajabu kweli. Nikitaka kufahamu KMC imejipangaje kwa mechi zinazofuata nitatakiwa kumsikiliza Anwar Binde na sio Jackson Mayanja, na nyombo vya habari vinapenda hili.
Nchi inabidi ipitie mabadiliko, vilabu inabidi vibadili uendeshaji wao na lazima turejee kwenye misingi ya kuwapa wachezaji thamani. Manara na mimi hapa tunakula kutokana na anachokifanya Jonas Mkude au Feitoto uwanjani, tunaishi kutokana na magoli ya Ditram Nchimbi au uhodari wa Juma Kaseja.
Katika dunia inayozunguka kweye mhimili wake ni muhimu hawa wawe na chapa imara kuliko wasemaji au waandishi, lazima wawe wakubwa zaidi.
Bahati mbaya ni kuwa tumeamua kuwabatiza wasemaji, tumeamua wawe wakubwa zaidi. Tumeenda mbali na kuhisi waandishi wana nguvu zaidi na wanafaa kutukuzwa. Kwenye tabasamu la Haji Manara kwa kila ubalozi anaopata kuna huzuni kubwa ya Miraji Athumani ambaye bao alilofunga linampa thamani mwandishi anayesimulia kuliko yeye aliyesababisha liwe simulizi.
Atamaliza maisha yake Simba na hatakuwa na thamani tena wakati mdomo wa Maulid Kitenge au Oscar Oscar ukiendelea kufanya kazi mpaka wapate mvi. Vilabu lazima virejee kwenye misingi ya kuwakuza wachezaji na hawa watasukuma mashabiki ndani ya uwanja. Lazima niwe na hamu ya kumuona Meddie Kagere kuliko kusubiri apambwe na maneno ya Haji Manara.

Advertisement