Sio Zengwe: Kumuangalia Aussems kwa jicho la pili

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-Sio Zengwe-Kumuangalia-Aussems-SimbaSC-jicho-pili

 

By Angetile Osiah

WIKI ilee niliandika kuhusu kiungo nyota wa Simba, Jonas Mkude hakuwa na tatizo la kinidhamu bali aliruhusiwa na klabu yake kwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia.
Nilisema kama hakuna zengwe, hicho ni kitu kizuri kwa sababu kinaondoa ule ubashiri ambao huwa unaenea kuhusu kutoonekana kwa mchezaji fulani.
Na wiki iliyopita niliandika kuhusu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa, ambaye wasifu na historia yake vilitosha kunishawishi kuwa ni mtu sahihi kuongoza klabu inayotaka kupiga hatua kubwa kama Simba na nikapendekeza jinsi soka la Bongo linavyoweza kuweka mikakati ya kuchota ujuzi wake.
Wiki hii nimesikia moja ya maamuzi makubwa ya kwanza katika uongozi wa Senzo; kumtimua kocha Patrick Aussems kwa sababu kadhaa, zikiwemo za kushindwa kudhibiti nidhamu katika timu yake, kushindwa kuonyesha nidhamu yeye mwenyewe alipofanya safari inayosadikika kuwa ya kwenda Afrika Kusini kusaini ajira mpya, kushindwa kuivusha timu hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika katika mwaka wake wa pili na pia kushindwa kutoa ushirikiano alipoitwa kujieleza.
Ni uamuzi mzito ambao kiongozi yeyote ambaye kweli anataka mabadiliko, ni lazima afanye hata kama unaumiza, ukizingatia rekodi za Aussems katika kipindi cha chini ya miaka miwili aliyokaa Simba.
Unamfukuzaje kocha ambaye msimu wa kwanza tu aliifikisha timu juu ya malengo aliyowekewa, yaani kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika katika mwaka ambao alitakiwa kuifikisha timu hatua ya makundi tu.
Kama kiongozi mwoga huwezi kufikia uamuzi kama huo katika kipindi ambacho kocha bado anaendelea kufanya vizuri akiwa amepoteza mchezo mmoja na kutoka sare mmoja na timu iko kileleni.
Kwa kuwa na msimamo kama huo, huwezi kuacha kuupongeza uongozi hata kama hapo baadaye uamuzi huu utaonekana haukuwa sahihi. Kufanya kile unachoamini ni sahihi bila ya kujali mazingira yasiyo sahihi yanayoweza kukukwamisha, ni kitu kikubwa.
Lakini naangalia sababu za kumtimua, naona kama zililundikwa na kutafutiwa pa kutokea, yaani ile meseji aliyotuma akiwa uwanja wa ndege kuwa anaondoka kwa mambo yake binafsi, ndiyo iliyowapa viongozi sababu nzito za kumshughulikia.
Maana kama kutofuzu hatua za awali za Ligi ya Mabingwa ni muda mrefu sana umepita tangu Simba iondolewe na UD Songo ya Msumbiji. Kama mkataba wake ulisema hivyo, basi leo tangu miezi mitatu iliyopita Aussems hangekuwa katika orodha ya makocha wa Ligi Kuu ya Bara.
Baada ya mechi zile mbili, uongozi ungekaa naye mezani na kumwambia amefeli kutimiza malengo aliyopewa kwenye mkataba wake na hapohapo kuuvunja. Nini kiliufanya uongozi usubiri muda wote huo hadi ulipopata ile meseji ya uwanja wa ndege?
Suala la kutosimamia nidhamu ya wachezaji nalo ni kama limedakwa tu na uongozi. Yaani kocha ndiye anayetakiwa kushtaki au kuchukulia hatua wachezaji watovu wa nidhamu.
Kocha ndiye anayekuwa na wachezaji kwa muda mwingi na anaiangalia nidhamu yao kwa kadri wanavyofika uwanjani kwa wakati na kutimiza maelekezo yote anayowapa. Hayo masuala kwamba walichelewa kulala eti kwa sababu walikuwa katika starehe, si masuala ya kocha.
Kocha ataangalia jinsi wanavyoshindwa kutimiza maelekezo yake ndipo atakapojua mchezaji wake hawezi kuingia kwenye kikosi cha kwanza; iwe ni kwa sababu amepoteza nguvu baa au mgonjwa, hilo ni suala jingine.
Anachoweza kufanya ni kuzungumza naye kwa karibu na kumueleza jinsi anavyoshuka kiwango an hivyo ajiangalie, la sivyo anaweza kupoteza namba kabisa kikosini. Ni kazi ya wale wanaompenda kumwambia kipenzi chao kuwa mpira ndio unaomuweka mjini hivyo apunguze starehe.
Isitoshe, utovu wa nidhamu haushuki siku moja kama mvua ya wakati wa kiangazi, ni suala la muda. Yaani hapo suala hilo lililundikwa kwa miezi kadhaa ndipo Aussems alipoonekana eti kwamba anashindwa kudhibiti nidhamu. Kwa hiyo wakati wote huo nidhamu inaanza kushuka, viongozi hawakuwa wanaona?
Cha msingi hapa ni mamlaka ya kocha kuhusu nidhamu yaliingiliwa. Huenda kile ambacho viongozi wanaona kuwa ni utovu wa nidhamu, kwake si jambo baya. Kwamba aingie kambini na wachezaji wachache au wachezaji wasikae kambini, ni jambo ambalo halitakiwi kuangaliwa kwa mtazamo hasi. Hawa wachezaji wanalipwa kwa kucheza mpira, au kwa maana nyingine ni professional kwa hiyo kuanza kuwalea kama wanafunzi wa sekondari eti kwa sababu wachezaji wa Bongo hawajidhibiti wanapokuwa huru, ni kuendekeza uzamani katika usasa.
Kama Simba imekubali mabadiliko, ikubali pia kubadilika katika masuala ya uratibu wa wachezaji. Huenda hilo nalo ni moja ya matatizo yanayozuia wachezaji wetu kuwa professional wa kweli.

Advertisement