Hii vita ya namba Simba SC, Yanga tema mate chini

Tuesday January 14 2020

Mwanaspoti-Simba SC-Yanga-Michezo-Mwanasport-MICHEZO Blog-Tanzania

 

By THOMAS NG’ITU

Dar es Salaam. KLABU za Simba na Yanga msimu huu zimeonyesha kabisa kwamba hazina masikhara baada ya kuamua kufanya usajili mkubwa ili kuwa na vikosi vipana.
Simba tangu mwanzoni mwa msimu walikuwa wakitamba kwamba wana vikosi viwili baada ya kudaka saini za nyota kadhaa kama Francis Kahata, Sharaf Eldin Shiboub, Deo Kanda, Ibrahim Ajibu, Beno Kakolanya, Miraj Athuman na Wabrazili watatu, Gerson Fraga, Wilker da Silver na Tairone da Silva.
Wakati huo upande wa Yanga nao walifanya usajili wa nyota kama Patrick Sibomana, Sidney Urikhob, Issa Bigirimana, Juma Balinya, David Molinga, Mapinduzi Balama, Ali Sonso, Ali Ali, Faruk Shikhalo na dirisha dogo wakapambana kupata saini ya Ditram Nchimbi.
Usajili mkubwa kwa timu zote mbili unazaa ushindani mkubwa wa namba. Ukizubaa tu imekula kwako.
Mwanaspoti limeangazia timu hizi mbili namna ambavyo zinavyowaingiza wachezaji wake katika vita.
 
AISHI MANULA VS BENO KAKOLANYA
 Simba wamebadilisha makipa mfululizo chini ya Manula. Amepita Deogratius Munishi ‘Dida’ na Said Mohamed ‘Nduda’, lakini msimu huu picha limekuwa tofauti tangu walipomsajili Beno Kakolanya ambaye alikuwa na msimu mzuri akiwa na Yanga kabla hajaamua kuwakacha na kukaa pembeni.
Kakolanya tangu amejiunga na timu hiyo amecheza mechi tisa hadi sasa na ameonyesha kiwango kikubwa.
Baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Yanga katika mechi ya Dabi ya Kariakoo, mashabiki walianza kuimba “tunamtaka Kakolanya” wakionyesha kupoteza imani na Manula, licha ya kwamba kiufundi hamna bao kati ya mawili hayo ambalo kusema ni makosa ya kipa. Vyovyote iwavyo, vita ya Na.1 Simba si ya kitoto.
 
FARUK SHIKALO VS METACHA MNATA
Makipa hawa wote ni wa timu za Taifa, Metacha ameitwa mfululizo katika kikosi cha Tanzania huku Faruk yeye akiitwa katika kikosi cha Kenya.
Ushindani wao katika kikosi cha Yanga ni mkubwa mno kutokana na wote wawili kuwa katika viwango bora na ndio maana kila mmoja anapopata nafasi huamua kufanya kweli.
Faruk ni kama amejihakikishia namba baada ya kuokoa hatari nyingi dhidi ya Simba na kuwabakisha Yanga mchezoni hadi wakapata sare ya 2-2.
 
ANDREW VICENT VS ALLY MTONI ‘SONSO’
Kukosekana kwa Dante mwanzoni mwa msimu kulimfanya Sonso acheze pacha wa Yondani katika nafasi ya ulinzi wa kati ya Yanga. Na hata anacheza kama beki wa kushoto bado anafanya kazi yake vizuri.
Wawili hawa wamekuwa ni wakabaji wazuri au huitwa beki namba 4 kwani Lamine Moro na Kelvin Yondani huwa wanatambulika kama beki namba tano.
Hivyo Sonso na Dante kutakuwa na kazi kubwa kwani kwenye mchezo wa Simba na Yanga, Sonso alianza na Yondani alicheza vizuri na hata alipoingia Dante ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu kumaliza mgomo wa maslahi, bado alifanya vizuri na kuonekana wazi kutakuwa na kazi ya ziada mtu kucheza.
 
TAIRONE SANTOS, KENNEDY JUMA VS
ERASTO NYONI
Hapa kuna utata kweli katika msimu huu hasa baada ya kuja kocha Sven Vandenbroeck ambaye ameonekana kuhitaji zaidi beki mrefu wa kati na mmoja mfupi.
Hali hiyo imemfanya Nyoni aondolewe katika kikosi cha kwanza ambapo ilizoeleka yeye kucheza na Pascal Wawa, lakini hivi sasa anacheza Kennedy na Wawa au Tairone na Wawa.
 Nyoni muda huu anajipanga kuhakikisha kwamba anafanya kitu mara mbili na zaidi ambacho kinafanywa na Tairone pamoja na Kennedy ili kuhakikisha anarejea katika kikosi cha kwanza ambacho anaonekana anakosa nafasi ya kuanza.
 
MAPINDUZI BALAMA VS FEISAL SALUM
Katika eneo la kiungo klabu ya Yanga patakuwa na patashika kwani ujio wa Mapinduzi Balama ni kama unamkosesha amani kiungo Feisal Salum ambaye alikuwa akipata nafasi mbele ya kocha wa zamani Mwinyi Zahera.  
Balama amezidi kuwa bora kadri siku zinavyozidi kwenda mbele huku upande wa Feisal kukiwa na ukimya kutokana na kutopata nafasi ya kutosha uwanjani.
Bao la kwanza alilofunga Balama kwa kuachia roketi la masafa marefu dhidi Simba, ambalo liliwarudisha Yanga mchezoni baada ya kutanguliwa 2-0 na kupata sare ya 2-2 linamfanya awe kipenzi cha Wanajangwani. Mambo kwa Fei yanatarajiwa kuwa magumu kwani viungo wengine Abdulaziz Makame na Mohamed Issa ‘Banka’ wanafanya vizuri kikosini.
 
JONAS MKUDE VS GERSON FRAGA
Kwenye eneo la kiungo ukabaji pale Simba moto unawaka tayari. Jonas Mkude yuko katika ubora wake huku Gerson Fraga naye akizidi kuchanganya.
Ukongwe wa Mkude umekuwa ni nguzo muhimu katika kikosi cha Simba lakini uwepo wa Fraga umeanza kumtishia Mkude kwani watu wameanza kumuelewa Mbrazil huyo.
Wakati huo huo kiungo mwingine Mzamiru Yassin ambaye amekuwa akifanya vizuri kwa hivi karibuni naye atakuwa na kazi ya ziada kwani ugumu wa namba umeongezeka.
 
JOHN BOCCO VS MEDDIE KAGERE
Kocha mpya wa Simba, Sven Vandenbroeck ameonekana kutumia mfumo 4-5-1. Katika mfumo huu anakuwa anamtumia mshambuliaji mmoja peke yake.
Hali hii itawafanya Meddie Kagere na John Bocco kuingia katika vita ya namba huku wote katika msimu uliopita wakitumika kama washambuliaji wakianza pamoja.
Pacha yao ilionekana kuwa bora hali iliyomfanya kocha wa zamani, Patrick Aussems kupiga kelele kwamba kukosekana kwa Bocco amekuwa akimtumia Kagere peke yake.
Sven pengine anaweza akaonyesha umma ni wapi Aussems alikuwa anakosea.
 
DITRAM NCHIMBI VS
YIKPE GNAMIEN
Huu wote ni usajili uliofanywa katika dirisha dogo la usajili, lengo kubwa ni kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo lilionekana kuwa na changamoto mwanzoni mwa msimu.
Uwapo wa wachezaji hawa unawafanya waingie katika vita ya namba kutokana na aina yao ya uchezaji kufanana, hivyo juhudi ya kila mmojawapo ndio itakayomfanya acheze.
Nchimbi na Yikpe wote ni wachezaji ambao wanatumia nguvu zaidi na kupiga mashuti, lakini Nchimbi kinachombeba ni kuanza kukubalika mapema mpaka kusajiliwa huku Yikpe akifanyishwa majaribio.
Hata hivyo, Nchimbi amekaririwa na gazeti hili kwamba anaamini akicheza na Tariq Seif anakuwa bora zaidi kutokana na aina ya ucheza wao kuendana kwa namna moja ama nyingine.

Advertisement