Sholo Mwamba, Msaga Sumu, Mzee wa Bwax wameishika singeli

Muktasari:

Ukiachana na muziki huo wa kizazi kipya  Bongo kuna muziki wa Singeli, ambao ulianza kuimbwa mitaani na awali mashabiki wake wengi walionekana kuwa wale wahuni na vijana mbalimbali ambao hawakuwa na shughuli za kufanya

KATIKA muziki wa kizazi kipya wapo wasanii wengi hapa nchini wanaotamba katika uwanja huo. Na haraka haraka huwezi kuwaacha kuwataja Diamond Platinamz, Ali Kiba, Vanessa Mdee, Ommy Dimpoz, Darasa, Harmonize, Nandy na wengineo wengi.
Ukiachana na muziki huo wa kizazi kipya  Bongo kuna muziki wa Singeli, ambao ulianza kuimbwa mitaani na awali mashabiki wake wengi walionekana kuwa wale wahuni na vijana mbalimbali ambao hawakuwa na shughuli za kufanya.
Jambo hilo kwa sasa si kweli kwani muziki huo wa Singeli umekuwa kipenzi hata kwa watu mashuhuri ambao wamekuwa wakiufatilia na kushabikia kama ulivyo muziki mwingine wa Ragger, Bongo Flavor,  Dansi na Bolingo.
Katika miaka hii miwili ya Singeli kuna wasanii watano ndio wamekuwa kama alama ya muziki huo kutokana na kufanya vizuri katika nyimbo zao  wanazoziachia mara kwa mara lakini hata uwezo wa kufanya shoo kubwa mbalimbali za hapa nchini.
Makala haya yanakuletea wasanii watano wanaofanya vizuri katika Muziki wa Singeli ambao umekuwa na wapenzi wengi hapa nchini katika lika mbalimbali lakini kama haitoshi umekuwa ukifatiliwa na watu wengi ambao wengine awali walikuwa wakiubeza.

MEJA KUNTA
Ameibuka mwaka 2019, katika Singeli na wimbo wake wa kwanza ambao uliwakamata watu wengi mtaani na kuanza kuimbwa katika maeneo mbalimbali kama vile katika vibanda vya kukodisha mikanda ya video, vijiwe vya bodaboda na maeneo mengine mengi.
Meja Kunta ambaye alikuwa akiimba katika shughuli za mitaani kama vile harusi, kuzindua makempu, kumtoa mtoto mdogo ndani (Hakika), alipata umaarufu baada ya kuimba Wimbo wa Mamu ambao ulikuwa ikiimbwa mpaka na watoto wa dogo mitaani.
Baada ya wimbo huo kusambaa katika maeneo mbalimbali akaanza kupata mialiko kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kuandikwa katika mitandao ya kijamii.  Katika kuonesha kwamba muziki wake umekuwa alikuwa akipata kazi ya kutumbuiza katika matamasha makubwa hapa nchini.
Kadiri siku zilivyozidi kwenda  Meja Kunta alizidi kukua na kufanya shoo kubwa kama za Fiesta, Wasafi Festival, Muziki Mnene na matamasha mengine mengi lakini sambamba na hilo anaendelea kutamba wakati huu na nyimbo zake za Acha Nilewe, Marioo, Naumia na Moyo, Nenda Ukalale, Haloo na Shori.
Katika kuona muziki wa Kunta unazidi kuwa mkubwa amefanya wimbo remix ya wimbo wa Mamu na msanii wa muda mrefu na maarufu hapa nchini wa kizazi kipya Mr Blue ambao nao umekuwa ukipigwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

MZEE WA BWAX
Mwanzoni mwa mwaka 2019, ndipo alipoanza kufanya vizuri baada ya kuachia Wimbo wa Kisimu Changu, ambao ulikuwa ikipendwa na watu wengi ambao walikuwa wakiimba wimbo huo katika maeneo mengi.
Bwax alionekana kuvuma na kusikika zaidi kwani aliweza kufanya wimbo mmoja na msanii wa kizazi kipya, Shelta, iliyotambulika kwa jila la Uswahilini, ambao nayo ulifanya vizuri kwa kupigwa katika vyombo mbalimbali vya habari.
Kama haitoshi Bwax aliitwa katika shoo kibao na kutumbuza vyema nyimbo zake na kuwafanya mashabiki kuimba naye mwanzo wa shoo hadi mwisho wake. Shoo hizo zikiwemo zile kubwa hapa nchini za Wasafi Festival, Muziki Mnene na Fiesta Festival.
Kwa sasa ukitaja wasanii wakubwa ambao wanaubeba Muziki wa Singeli na kufanya vizuri katika nyimbo zao, shoo na masuala mengine huwezi kuacha kumtaja Mzee wa Bwax, kwani anafanya vizuri na yimbo zake mpaka kupendwa na viongozi wa nchi.
Miongoni mwa nyimbo ambazo amezitoa Mzee wa Bwax na kufanya vizuri mpaka sasa ni Kisimu Changu, Sanamu la Michelini, Kisulisuli, Unaringa una Nini, Naipenda Yanga na Vikao.

SHOLO MWAMBA
Awali alionekana kama anashindana na msanii mwenzake wa Singeli, Man Fongo, lakini haikuwa hivyo kwani amezidi kupandisha thamani ya muziki wake na kuwa kubwa kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele katika muziki huo ambao nao unazidi kukuwa hapa Tanzania.
Mwamba ni miongoni mwa wasanii wanafanya vizuri katika Muziki wa Singeli na nyimbo zake mbalimbali ambazo amekuwa akiziachia miongoni mwa hizo hizi zinazozidi kutamba ni Ghetto la Bibi, Kimbia na Anataka Uma.
Nyimbo nyingine za Sholo Mwamba ambazo zinatamba ni Ukinipa Sisemi, Kama Ronaldo, Namba Moja na Mama ambazo zinamfanya kuwemo katika matamasha makubwa ya Feista, Wasafi na Muziki Mnene na kila akipanda jukwaani mashabiki wengi ni kama wanachizika vile.
Mashabiki hao huwa wanachizika na Sholo Mwamba kutokana na kuimba naye nyimbo kwa pamoja, kucheza naye na wengine hunogewa mpaka kuamua kuvua mashati na kucheza huku majasho yakiwamiminika.


DULLAH MAKABILA
Alianza kusikika na kufatiliwa na wapenzi wa Mujziki wa Singeli baada ya kuachia wimbo wake wa Haujaulamba, ambayo ilikuwa ikiimbiwa katika maeneo mengi kama katika vyombo vya habari, bodaboda na vibanda vya kukodisha na kuuza CD, na maeneo mengine mengi.
Makabila ambaye kwa sasa amekuwa akifanya shoo nyingi kubwa na ndogo ni miongoni mwa wasanii wa Muziki wa Singeli ambao wanatamba na kufatiliwa na wapenzi wengi lakini kama haitoshi amekuwa akifanya mahojiano mara kwa mara na vyombo vya habari.
Makabila kwa sasa anatamba na nyimbo za Kuingizwa, Demu Wako Namba Ngapi, Waongo, Mtoni Kumedamshi na Dua.

MSAGA SUMU
Ni miongoni mwa waanzilishi wa Muziki wa Singeli na kwa mara ya kwanza aliachia wimbo wake ilikuwa 2007, ambapo ni kama alikuwa anautambulisha  katika anga la burudani muziki huo ambao ulikuwa bado hauna wapenzi wengi waliokuwa wakiufatilia zaidi ni wale waliokuwa wakiishi uswahilini.
Wimbo huio ambayo aliachia Msaga Sumu ilikuwa ikitambulika kama Mama wa Kambo, ambayo ilikuwa nzuri kutokana na ujumbe uliokuwa ndani yake.  Na tangu hapo wakaibuka wasanii kibao kuna ambao walifanya vizuri na wengine walikuja kuzuga tu.