Msuva kiroho safi kwa Sadio Mane kutwaa tuzo CAF

Muktasari:

Msuva anayehusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno, alizifuatilia tuzo hizo zilizofanyika Hurghurda, Misri huku tamanio lake ni kuona tuzo hiyo itaenda kwa Sadio Mane wa Liverpool na Timu ya Taifa ya Senegal, jambo lililokuwa kweli.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayeichezea Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, amesema Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka 2019 imeenda kwa mtu sahihi kwani Sadio Mane aliistahili.
Msuva anayehusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno, alizifuatilia tuzo hizo zilizofanyika Hurghurda, Misri huku tamanio lake ni kuona tuzo hiyo itaenda kwa Sadio Mane wa Liverpool na Timu ya Taifa ya Senegal, jambo lililokuwa kweli.
“Amekuwa na mwaka bora na wenye mafanikio katika ngazi zote, ukiangalia ameisaidia Liverpool kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, unaweza kusema alikuwa na Salah ni sawa wote walikuwa wachezaji muhimu lakini cha kuwatofautisha Mane aliifikisha fainali Senegal katika Afcon,” alisema Msuva.
Mane, 27, ametwaa tuzo hiyo kwa mara yake ya kwanza baada ya kumaliza katika nafasi ya pili katika miaka miwili mfululizo, 2017 na 2018, nyuma ya mchezaji mwenzake wa Liverpool, Mohamed Salah. Mwaka 2016 alishika nafasi  ya tatu.
Nyota  huyo, amekuwa mchezaji wa pili katika historia ya taifa lake, kutwaa tuzo hiyo kubwa Afrika baada ya  El Hadji Diouf, ambaye  alifanya hivyo miaka ya 2001 na  2002.
Katika tuzo zilifanyika usiku wa Jumanne, Bendera ya Tanzania ilipeperusha  na  Mwanabongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye alinogesha sherehe hizo kwa kutumbuiza kibao chake cha Yope remix alichoshirikiana na  Innoss’B.