Mashabiki Bandari wapiga nduru

Saturday January 11 2020

Mwanaspoti-Mashabiki-Kenya-Bandari-Tanzania-wapiga nduru-LigiKuu-

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. MASHABIKI wa soka wa jimbo la Pwani jana walipiga nduru kuwataka wachezaji wa Bandari wajitume na kuhakikisha wameondoka uwanjani Mbaraki Sports Club na ushindi hapo kesho Jumapili timu hiyo itakapocheza na Tusker FC kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Mashabiki hao waliotoka sehemu mbalimbali za jimbo hilo wametuma jumbe zao kwa Mwanaspoti wakiwataka wanasoka wao wafanye kila wawezavyo kuhakikisha wamepata pointi zote tatu na wapinzani wao wa Tusker waondoke kurudi makwao mikono mitupu.
Ramadhan Omar wa Mtwapa anasema katika ujumbe wake kuwa Bandari inaweza kufanya vizuri na kushinda mechi nyingi za mkondo wa pili kwani wana wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanaocheza soka la hali ya juu. “Nilipoishuhudia timu yangu ilipocheza mechi mbikli za nyumbani zilizopita, nina imani hata kama Tusker wako kileleni mwa ligi, twataka vijana wetu wawashinde na kuwarudisha nyumbani wakiwa hawana la kufanya,” akasema Omar.
Shadrack Mwakatika kutoka Mwatate anasema ameonelea vizuri kama Bandari watajitakasa hivi leo kwa kuwashinda Tusker na hilo lawezekana kwani ingawa wageni hao wako kileleni mwa ligi, hawawezi kuwashinda vijana wa nyumbani.
“Nionavyo mimi vijana wetu hivi sasa watakuwa sawa na walikuwa wakishindwa kwa sababu ya kucheza mechi nyingi zikiwemo za Afrika Mashariki na Caf Confederation Cup,” akasema Mwakatika ambaye anaamini Bandari kutoka uwanjani na ushindi wa zaidi ya mabao mawili.
Salim Kassim wa Msambweni anaamini kama Bandari itafanya uteuzi wa wachezaji wa jimbo la Pwani ama kuchaguwa wanasoka wa Bandari Youth, timu itakuwa imara zaidi. Lakini dhidi ya Tusker, Kassim anasema: “Ushindi ni wetu, wanabia hawatuwezi.”

Advertisement