Magori: Kwa Simba hii Ajibu, Chama wajipange

Muktasari:

Simba hii anaweza kuja na kukaa benchi, ukigundua mwaka jana hatukuwa hivyo, tulikuwa tunabembeleza baadhi ya wachezaji, wakikosekana mnaumwa hili tumefuta tumekuwa na timu moja

Dar es Salaam. Katika mfululizo wa makala za mahojiano maalum na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba na sasa mshauri wa bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji’, Crescentius Magori alieleza kuhsuu kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, usajili na changamoto ya nidhamu ndani ya kikosi.
Leo katika muendelezo wa makala yake, kigogo huyo mwenye uzoefu na masuala ya soka anaeleza kwa kina usajili uliofanywa Simba msimu huu. Bila kificho Magori anasema usajili huo ni bora na kwamba, unaweza  kuwapoteza hata wale wanaodhaniwa ni wakali zaidi. Kivipi? Endelea...!

VIPI USAJILI SIMBA
“Siwezi kusema tunakosea kusajili, unajua usajili ni kama kamari kuna wakati unaweza kufanikiwa ama ukakosea, kwa mfano mchezaji tuliyemtarajia makubwa kutoka kwake ni Salamba (Adam), aliletwa la Lechantre (Pierre). Alimuona akiwa Lipuli na akampendekeza asajiliwe kwa kuwa ni mdogo, ana nguvu akitaka kumtengeneza zaidi akiwa Simba.
“Bahati mbaya Lechantre alimaliza mkataba wake na kuondoka baadaye akaja Aussems (Patrick). Salamba akaanza kupotea na kocha akasema amejaribu kumtengeneza, ila hafikii ubora anaoutaka. Sisi kama viongozi tutafanya nini hapo? Tukakubaliana tumtoe kwa mkopo bahati nzuri amepata timu huko nje Kuwait tumemruhusu akajaribu bahati yake.
“Sasa unaweza kuchanganyikiwa na huenda Lechantre angebaki Salamba angeng’ara kwani ndiye aliyempendekeza, hivyo nikisema Simba imekuwa ikibadilika kwa matokeo chanya kila siku inavyosogea na mapungufu ni machache huwa namaanisha kuna mengi mazuri kwenye usajili.
“Niwaambie ukweli kuna wachezaji unaweza kuwaona ni mastaa katika klabu zao, lakini wakija Simba hawawezi kupata nafasi kirahisi. Ili ucheze Simba unahitaji kujituma kwa hali ya juu kulingana na timu ilivyo.
“Unaweza kumuangalia Ajibu (Ibrahim) si alikuwa nyota kabisa kule Yanga na wakimkosa wanaumia vichwa? Lakini akija hapa Simba anatakiwa kujituma haitakuwa rahisi kwake kupata nafasi mara kwa mara, Simba hii unaweza kuangalia hata sasa katika mechi tulizocheza kuna mtu amemkumbuka Chama?”
“Mambo yanakwenda kama vile hayupo, maana yake ni kuwa, msimu huu tumeamua kutengeneza timu na sio kumtegemea mchezaji mmoja. Kila mchezaji kikosini anacheza na matokeo tunapata kuna wakati hata kocha anaumiza kichwa kupanga timu,” anasema na kuongeza; “Watu wanaweza kumshangaa hata Ndemla (Said) anapata tabu kupata nafasi, si kosa lake ni kutokana na kuenea kwa timu. Lakini, akiondoka akaenda kwingine anaweza kuwa staa mkubwa na watu wakashangaa. Nilimuangalia Mkude (Jonas) alivyocheza kule Sudan, lakini Simba hii anaweza kuja na kukaa benchi, ukigundua mwaka jana hatukuwa hivyo, tulikuwa tunabembeleza baadhi ya wachezaji, wakikosekana mnaumwa hili tumefuta tumekuwa na timu moja.”

KIKOSI KIPANA
Magori anasema lengo la kufanya hivyo ni kutaka Simba iwe na kikosi kipana na cha ushindani.
“Tulijitahidi kila nafasi tutengeneze uimara wa zaidi ya wachezaji wawili, anzia langoni mpaka kule mbele kidogo tulikuwa na shida katika beki namba mbili tuna Kapombe (Shomari), ambaye bado hajarudi katika kiwango chake ingawa tuna Shamte (Haruna) ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda kunolewa, sasa kinachohitajika ni nidhamu bora na uwajibikaji tu.

KUITOSA MAKAO MAKUU SIMBAZI
Kuhusu viongozi wa Simba kutofanya kazi zake za kila siku kwenye makao makuu ya klabu yaani Mtaa wa Msimbazi, Magori anaeleza sababu za msingi:
“Kwanza pale hapawezekani, nilijaribu kwenda pale kama mara mbili au tatu nikagundua hapawezekani. Kwanza kuna kelele, yaani zogo moja kwa moja na huwezi kufanya kazi pale. Pili, nafikiri ushauri wangu kwa bodi, pale ni bora iwe nyumba ya klabu au iwe nyumba ya biashara kisha nyumba ya utawala halafu ya tatu ofisi za ufundi ziwe kule Bunju yaani Simba iwe na ofisi tofauti tatu.
“Pale Msimbazi hakuna hata maegesho ya magari, sasa chukulia unamleta mdhamini unamletaje hapo? Barabara ya mwendokasi ipo mpaka chini pale maana ofisi zile zipo pale Kariakoo katikati kabisa. kinachowezekana pale ni kuwa nyumba ya klabu kwa kuwa wanachama ni rahisi kufika.
“Pale wanapata huduma za kiuanachama na pia kufunguliwe maduka makubwa kwa kuwa ni rahisi kufikika kutokana na asili ya eneo lenyewe ni kibiashara. Kama nilivyosema unaweza kufanya kukawa sehemu ya kibiashara chini ukatengeneza maduka na juu ikawa hoteli ama ukajenga ofisi watu wakapanga.”

MALENGO YA SIMBA
“Binafsi niseme ukweli kwamba, kwa Simba hii unatakiwa kushinda mechi zote, kama mambo yote yakiwa sawa, sijui nisemeje? Nilikuwa nazungumza na Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa hivi karibuni, ampangie malengo Aussmes kwamba, timu tuliyonayo tunatakiwa tushinde mechi zote 38.
“Kwa sababu Simba ni tofauti kabisa na klabu zingine za Ligi Kuu Bara. Ni timu kubwa sana, hivyo wachezaji wakitoa uwajibikaji wa asilimia 100 kwa kila mechi ukiongeza na ushindani wa nafasi wa ndani ya timu, unaweza kuona unakosaje ushindi.
“Nendeni hata mkaangalie mazoezini, timu yetu ushindani ni mkubwa sana hata wanapocheza wenyewe kwa wenyewe. Sasa kwenye mazoezi Kagere (Meddie) anakutana na mtu kama Tairone au Nyoni (Erasto) anafunga hapo halafu unamleta kwenye mechi anakutana na beki laini unafikiri atafanyaje?
Wanaweza kukutana na timu ngumu labda wakikutana na Yanga au Azam, lakini hizi zingine ni rahisi tu. Nafahamu kuwa ni ngumu kushinda mechi zote 38, lakini kocha anapaswa kujaribu kuvunja rekodi na kama timu wakikubaliana kuweka rekodi ya kucheza bila kupoteza inawezekana.