Harmonize atasindikizwa Mtwara na Zari, Wema, Mobeto mlevi kasema

Tuesday December 31 2019

Mwanaspoti-Harmonize-Tanzania-atasindikizwa Mtwara-Zari-Wema-Mobeto mlevi kasema

 

TRENI la Diamond Platnumz a.k.a Mondi bin Laden limetikisa nchi. Hapa kijiweni, Dk Levy amekuja na nyeti kuwa Harmonize atasindikizwa Mtwara kwa helikopta mbili, meli, Bombardier mbili, vilevile atasindikizwa na Zari, Wema na Hamisa Mobetto. Hiyo story Luqman Maloto anaikataa.
LUQMAN: Arsene Wenger yuleyule aliyeipa ubingwa Arsenal wa EPL mara kibao, akaifanya Arsenal kuwa The Big Two England, ilikuwa Arsenal na Man United. Eti huyohuyo akafanya Arsenal kuwa timu mbovu na sisi tukaamini. Tangu Wenger alipoondoka Arsenal, yamekuwa majanga kupata kutokea. Kwa mara ya kwanza katika historia, Arsenal inafunga mwaka ikiwa nafasi ya 12.
Mashabiki walivyo watu wa hovyo, wakawa wanaingia na mabango “Wenger Out” wakati msiba wa timu ni mwanahisa mkubwa wa timu, Stan Kroenke. Tajiri bahili sijapata kuona. Kipindi Everton wanamchukua Carlo Ancelotti, Arsenal wanamtwaa Mikel Arteta. Arsenal hawapo serious. Sasa naamini mpaka Wenger alipotangaza kujiuzulu, ni baada ya kuona alikuwa anafanya kazi na nati.
DK LEVY: Moja kati ya matukio ya kuumiza. Kusikitisha. Kuhuzunisha. Kutafakarisha na kusononesha kama sio kuvuruga akili. Ni hili la Arsenal. Ni kama Mwalimu Nyerere kuondoka madarakani halafu nchi akakabidhiwa Steve Nyerere au Dk Shika. Daraja la Kocha Wenger ni kubwa sana. Lakini anakuja muuza mafenesi kurithi mikoba yake. Eti ‘Uhai Emely’ sijui. Anaondoka kocha wa dunia anakuja mpanga makopo wa Pep pale Man City bwana Arteta. Hizi simbilisi kama Freddie Ljungberg wakati wa Wenger zilikuwa zinacheza na watoto uani pale Colney London. Thierry Henry alitupwa na watoto pia kabla ya kuondoka na kwenda kufanya kibarua cha uchambuzi wa soka. Wenger alijua wale sio makocha. Ndo maana Henry alipokwenda Monaco aliishia kutia aibu. Leo hii Leicester City ina kocha mkubwa kuliko Arsenal. West Ham  imefukuza kocha mkubwa kuliko Arsenal. Everton inamiliki kocha mkubwa kuliko Arsenal.
Kucheza vizuri ujanani sio kuja kuwa kocha bora uzeeni. Uwezo wa soka wa Seleman Matola haukufikia kiwango cha Edibily Lunyamila. Lakini leo hii Sele ni mmoja wa makocha bora sana nchini. Unadhani Mecky Mexime alikuwa bora kuliko Pawassa uwanjani? Au Fred Felix Kataraiya Baba Isaya Majeshi Minziro alikuwa mkali zaidi ya Athumani China? Hapana. Ila wamekuja kuwa makocha bora sana. Kuwa Zidane au Pep Guardiola ni kipawa toka kwa Mungu. Yaani unakimbiza kwenye uchezaji kisha unafunika kwenye ufundishaji. Ogopa. Wale Arsenal ni maiti inayotembea bila jeneza.
LUQMAN: Yule Stan Kroenke anazidiwa akili, maarifa na MO Dewji. Jitu limetoka Marekani, halipendi soka, haliipendi timu, limeona fursa. Halijui biashara ya soka inavyokwenda, halafu linapewa timu kubwa kama Arsenal. Kuna kipindi Arsenal ilikuwa inaongoza kwa mapato England. Ikawa Tano Bora kwa utajiri duniani. Siku hizi Arsenal inazidiwa mpaka na Tottenham Hotspur. Yule Stan Kroenke ni msiba. Hovyo kupita kiasi. Arsenal ni ya kuongozwa na Mikel Arteta? Kweli? Wakati Spurs wana Mourinho.
DK LEVY: Stan Kroenke sio Mmarekani. Anaitwa Stanley Kilewo ni Mpare wa Ugweno huko. Mama yake kiasili anatokea Mwanga milimani kule. Moja ya sifa yake kuu ni ubahili. Wenger alimleta Vieira, Kanu, Marc Overmas, Emmanuel Petit, Wiltord, Henry, Ashley Cole, Edu na wengineo kibao. Ila timu ilipokabidhiwa kwa Mpare wa Ugweno tu sera zikabadilika. Kwa kisingizio cha deni la Uwanja wa Emirates. Wakaanza kuleta ndama badala ya ng’ombe kamili. Timu ikawa kama Nursery School. Ikawa kama Sunday School. Ikawa kama Madrassa. Ikawa ya Viben Ten na Viserengeti Boys tupu. Wakaanza kusajili kadi za kliniki badala ya wachezaji wa soka. Lakini kwa kuwa Wenger alikuwa anajua sana ndo maana mashabiki hawakuona tofauti. Kila msimu timu yenye Viben Ten inaingia nne bora EPL na robo fainali ya UEFA kila msimu. Mwisho wakagundua kuwa wao ni wasindikizaji ila maiti inazikwa na Sheikh. Miaka inakatika bila kunyanyua makwapa. Ndo yakaanza mabango ya ‘Wenger Out’ badala ya ‘Kreonke Go To Hell’. Leo ndo akili zinawakaa sawa na kugundua tatizo sio Mfaransa bali ni Mpare wa Ugweno anayeishi Marekani.
LUQMAN: Kweli Liverpool iliyowahi kuwa mufilisi kipindi cha Wenger, ndio hii inatisha haifungiki. Yule Stan Kroenke wala hana wivu. Haoni aibu kuifanya Arsenal kuwa nafasi nane za mwisho mwaka unakatika. Yule Stan Kroenke angekuwa Bongo tungempa kesi ya uhujumu uchumi. Aliikuta Arsenal ni klabu bora, ameifanya kuwa klabu ya hovyo. Kwa jinsi alivyoididimiza Arsenal, Kroenke kesi ya uhujumu uchumi inamhusu. Mmarekani pori yule.
DK LEVY: Angekuwa Bongo ningempakia kwenye treni la Diamond. Pale Itigi ningemshusha na kumtupa awe chakula cha fisi na kenge. Hana tofauti na waliofilisi mashirika ya umma nchini. Kama NMC, RTC, UFI, RETCO, Railways, KIUTA, TANCUT ALMASI, Tanganyika Packers na mengineyo kama Bodi ya Korosho. Au General Tyre pale Arusha. Angekuwa Wasafi angetimuliwa kama kina Kifesi. Kreonke alifaa kuwa Segerea kengepori yule. Watu wa vile hata enzi za manabii walikwamisha juhudi za watumishi na mitume wa Mungu. Kwanza ukimtazama vizuri nywele macho na ndevu zake unaona kabisa kijamaa ni Kifreemason. Soka kimevamia tu. Kinatunyonya damu kupitia maumivu ya ushabiki wa soka. Bila Wenger hiyo Arsenal ingeshuka daraja kabla watoto wetu hawajazaliwa.
LUQMAN: Umeliongelea treni la Diamond hapo, vipi umelihusudu? Si nilikwambia twende na Harmonize wako ukakataa? Hesabu mikoa ambayo treni la kati kwenda Kigoma linapita. Dar na viunga vyake, Moro na wilaya zake, Dodoma na vitongoji vyake, Tabora na miji yake. Kigoma na vijiji mpaka kata zake. Harmonize angepanda treni angeosha nyota. Eti na yeye anakwenda kukwea chopa kuwashukuru wana Mtwara. Sasa Wamachinga watamfaidi vipi akiwa kwenye helikopta. Dogo ana makuu kumbe.
DK LEVY: Unachotakiwa kujua ni kwamba Harmonize ana hofu ya Mungu. Ndo maana alikwepa kupanda treni la Mondi. Kwenye treni mule yamefanyika mambo mengi ya nuru na gizani. Kuna michezo ambayo mademu walikuwa wanasikia tu kwa mashosti zao kwenye treni wamefanya. Ulevi wa kila aina ya vilevi umefanyika. Mwache Konde Boy afanye kiungwana shughuli zake. Na hao ‘mabichi boi’ wako waendelee na ‘ubichi boi’ wao. Nguvu inayotumika na Mondi ni kwa sababu ya nguvu ya Konde Boy. Sasa umefanya nitoe siri za kambi. Konde Boy anaenda Mtwara na chopa mbili meli mbili na Bombadia mbili. Wakati ninyi mmewabebelea kina Rashida Wanjara sisi tunampeleka  Zari na Mobetto. Na tutawakalisha ndege moja na watoto wao na mabwana zao walionao hivi sasa tunawapakia pamoja. Na Wema Sepetu ndani. Ikibidi tunambeba na Mzee Abdul. Tutampitia pale Magomeni Kagera na chopa. Akagonge ngoma lake la Dudu la Yuyuu.
LUQMAN: Hivi kumbe Dudu la Yuyu hajaenda Kigoma? Meli, chopa, Zari, Mobetto, Wema. Hiyo ni story ya kweli au umemsikia mlevi akisimulia?
DK LEVY: Mimi ni Katibu Kiongozi wa Serikali ya Konde Gang. Hatuna tabia ya kuzusha stori ili kujipaisha. Ni vitendo tu ndo maana Tandahimba tumepewa jimbo.
LUQMAN: Sasa Diamond kwenye treni njiani alikuwa anakutana na watu wenye mabango, wanampungia kumsaliamia na kumfurahia. Sehemu nyingi alipiga shoo fupi kutuliza mzuka wa mashabiki, sasa huko kwenye meli Harmonize atakutana na nani baharini? Samaki na dagaa ndio watamshangilia?
DK LEVY: Ngoja upewe darasa. Vituo vya treni vilivyo na watu ni vile vya mijini tu. Yaani Moro, Dom, Itigi, Tabora na Kigoma. Pili Harmonize anaenda nyumbani kwao haendi kuzurura. Hafanyi ziara ya maonesho bali anaenda kufanya onesho kwao. Unachotakiwa kujua ni kwamba Diamond na watu wake wameenda mbali na jiji la Daslama. Konde Boy anavuka mikoa miwili tu kufika kwao. Hata angetumia treni bado asingekuwa na vituo vingi kama basi la mwendokasi kusalimia watu. Misafara ya kusimama njiani na kusalimia watu, Konde Boy kamuachia mwenye nchi (JPM) ambaye ndiye aliyempa  Jimbo la Tandahimba mpaka sasa. Kifupi, weka ugoko niweke jiwe.Advertisement