Pamzo ampeleka Olunga kwa Samatta

Thursday March 26 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Kenya, Pamzo ampeleka Olunga, Samatta, Japan katika klabu ya Kashiwa Reysol

 

By FADHILI ATHUMANI

KOCHA wa Posta Rangers, Sammy Pamzo Omollo, amemtaka straika wa Harambee Stars, Michael Olunga,, kurejea kwenye soka la bara Ulaya, na ikiwezekana Ligi Kuu ya England, anakochezea Mtanzania Mbwana wa Samatta wa Aston Villa.
Omollo, ambaye ni mmoja wa makocha wazawa wenye uzoefu wa muda mrefu, anaamini kwa ubora alionao Olunga, ambaye kwa sasa ndio mshambuliaji namba moja Kenya, hastahili kucheza nje ya ligi kubwa za Ulaya, kwani hakuna kinachomzuia kucheza soka la Ulaya.
Kocha huyo alisema hayo katika mazungumzo na Mwanaspoti mapema juma hili ambapo alimtaka nyota huyo anayecheza soka lake la kulipwa nchini Japan katika klabu ya Kashiwa Reysol inayposhiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo kuchangamka kabla hakujakucha.
“Unajua maisha ya mchezaji ni mafupi sana. Mwanasoka anapofika miaka 30 na kuendelea anakuwa hana umuhimu tena, ndio maana namshauri Olunga, achangamke na kurudi Ulaya, tunataka kumuona kwenye ligi kubwa kama EPL sio huko Japan,” alisema Pamzo.
Olunga, msimu uliopita alifunga zaidi ya mabao 27 na kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili huku ikipanda Ligi Kuu, lakini Pamzo anaamini hiyo haitoshi kwani ili aweze kuthibitisha ubora wake, ni lazima akapambane na waliobora zaidi yake.
Nyota huyo wa zamani wa Thika United, Tusker FC na Gor Mahia, tayari ameshafungua akaunti ya mabao msimu huu, akitupia kambani mara mbili, klabu yake ilipokutana na Consadole Sapporo (Februari 22). Pia amefunga bao dhidi ya Gambo Osaka, kwenye mechi ya J League.
Olunga alichezea Girona ya La Liga kwa mkopo 2018.

Advertisement