Ndolanga asimulia alivyomchapa waziri na alivyonusurika kifungo

Monday February 24 2020

Mwanaspoti, Ndolanga, asimulia, alivyomchapa waziri, Tanzania,kunusurika, kifungo

 

By Imani Makongoro

Ni zaidi ya miaka 10 imepita, lakini kumbukumbu ya kesi ya viongozi wa juu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), bado inajirudia kichwani kwa Muhidini Ndolanga, aliyekuwa kinara wa taasisi hiyo.
Ndolanga, rais wa heshima wa TFF na ambaye anakumbukwa kwa misimamo thabiti enzi ya uongozi wake FAT (sasa TFF), anasema hakimu alipomwambia hana hatia, hakuduwaa.
“Sikutaka kujua nini kitaendelea, niliondoka bila kugeuka nyuma,” alisema katika mazungumzo na Mwananchi wiki hii.
Kigogo huyo aliondoka akimuacha mahakamani katibu wake mkuu, Ismael Aden Rage na  Yonaza Seleki, aliyekuwa mhazini.
“Naikumbuka ile kesi, hakimu alinyanyuka kutoka kitini, karani akamwambia bado hujamaliza kutoa hukumu. Akarudi katika kiti, akaniambia sina hatia, niko huru, naweza kuondoka,” alisema Ndolanga.
“Sikutaka hata kugeuka nyuma. Nilishaambiwa sina hatia halafu niendelee kubaki mahakamani? Nasubiri nini? Niliondoka moja kwa moja kurudi nyumbani.”
Hata hivyo, Ndolanga anasema ilikuwa ni kesi ambayo mpaka leo anaamini ilikuwa ni ya kumchafua baada ya majaribio kadhaa ya kupinduliwa FAT kukwama.
“Serikali kupitia Kurugenzi ya Maendeleo ya Michezo ndiyo ilinishtaki. Ilikuwa ni kesi ya kunichafua baada ya kuona kila njia ya kuniondoa madarakani imeshindikana ndipo wakanipa kesi ile,” anasema Ndolanga.
Kigogo huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa FAT tangu mwaka 1993 hadi 2004, anasema  hakumbuki ilikuwa mwaka gani, lakini alishtakiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za FAT.
“Serikali ndiyo ilinishtaki niliambiwa nimetumia fedha za FAT vibaya nakumbuka nilizitumia kulipia huduma ya simu,” anasema.
“Mwanasheria wangu wakati huo, Kassim Nyangarika aliniambia ‘hii kesi nyepesi. Nenda Shirika la Posta, kaprint (kachapishe) kumbukumbu ya simu ulizopiga niletee’.
“Mwanasheria wangu akamwambia hakimu kuwa ‘alichofanya mteja wangu ni sahihi, sababu alilipia huduma ya simu ambazo ni za kazi anayoifanya na kutoa ushahidi katika ile fomu ya posta ambayo ilionyesha mawasiliano yangu yalikuwa kutoka Raha Tower kwenda TFF na Zurich, Uswisi yalipo makao makuu ya Fifa’.”
Katika utawala wake, mara kadhaa Serikali iliingilia kati masuala ya soka, ikiwa ni pamoja na kumuengua madarakani, lakini baadaye Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) likatishia kuivua Tanzania uanachama.
Hata ulipoundwa uongozi wa muda, Ndolanga aliupinga na baadaye Fifa kutoa maelekezo ya jinsi ya kuunda kamati ya uongozi iliyoshirikisha pande zote mbili zilizokuwa katika mgogoro.
Juhudi nyingine za kumtoa Ndolanga kwa kura zilishindikana kutokana na wapigakura kumuunga mkono hadi idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu ilipoongezeka na kura kulazimika kupigwa mara mbili ndipo alipoanguka.

Maisha ya Ndolanga FAT
Kiongozi huyo wa zamani wa Pan African anasema changamoto zilikuwa nyingi, lakini zilichochewa zaidi katika hafla ya kuiaga Prisons kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.
“Tulimualika aliyekuwa makamu wa rais, Dk Omari Ally Juma kuwa mgeni rasmi wakati wa kuiaga timu. Katika hotuba yake alisema FAT ni uozo mtupu, baada ya hafla ile Juma Kapuya (aliyekuwa waziri mwenye dhamana na michezo) alimuagiza Leonard Thadeo kuitisha mkutano wa kuijadili FAT.
“Tuliitwa Morogoro katika mkutano Kapuya alitangaza kuifuta Kamati ya Utendaji ya FAT, wala sikubishana naye nilirejea Dar es Salaam na kutuma fax Fifa kuhusu kilichotokea na Serikali kuingilia masuala ya michezo.

Fifa yashusha rungu
Anasema siku iliyofuatia mapema Fifa ilijibu kwa kuifungia Tanzania kutokana na tukio hilo.
“Mimi nikarudi zangu kijijini kwetu nikijipanga kugombea ubunge. Nikiwa kule nikapigiwa simu nirudi ili kujua hatima ya kifungo cha Fifa,” anasema.
“Iliundwa kamati ya watu watatu ambao ni Anna Abdallah, Joseph Mungai na Profesa Phillemon Sarungi kuchunguza jambo hilo na kupata mwafaka, nikaitwa.
“Katika kikao kile niliwambia kama mnataka tufunguliwe, basi mwambieni Kapuya aondoe kamati yake aliyoiweka FAT kwa kuwa hicho ndicho chanzo.
“Baada ya saa chache Kapuya akanipigia simu kuwa ameiondoa. Nikamwambia lete barua. Akaleta na siku iliyofuatia nikaiandika Fifa nikiambatanisha na barua ya Kapuya. Basi Fifa wakatufungulia.
Ndolanga anasema tangu hapo, Tanzania haijawahi kufungiwa kwa kuwa Serikali iliacha kuingilia soka.

Aiburuza BMT Mahakamani
Mzozo wake na mamlaka haukuishia hapo. Ndolanga pia anakumbukwa kulishtaki Baraza la Michezo la Taifa (BMT)  mahakamani.
“Jina langu liliondolewa katika orodha ya wagombea katika uchaguzi mkuu wa FAT. Wakati huo Said El Maamry alikuwa mwenyekiti wa BMT,” anakumbuka.
Aliamua kuishirikisha Fifa ambayo ilimuuliza kama ana uhakika atashinda kesi na jibu lake likawa ndio.
“Kweli nilishinda ile kesi. Si kweli kwamba masuala yote ya mpira hayapelekwi mahakamani, lakini kuna ishu na ishu,” anasema kigogo huyo ambaye enzi zake alibatizwa jina la Tyson.

Soka tangu utotoni
Ndolanga, ambaye alikuwa mkurugenzi wa wanyamapori, alianzia masuala ya uongozi wa soka akiwa Chama cha Soka Arusha.
“Nilikuwa nikipenda mpira tangu nikiwa shule ya Msingi Kitangali huko Newala,” anasimulia.
“Nilipofika darasa la tatu nikarudi kijiji nilichozaliwa cha Mkunya, lakini hakikuwa na shule, nikajiunga na shule kijiji cha pili cha Makuta huko huko Newala hadi darasa la nane.
Anasema baadaye alijiunga na Sekondari ya Tabora Boys kabla ya kujiunga na Chuo cha Mweka Moshi akijifunza utaalamu wa wanyama pori na kumalizia stashahada.
“Kote huko nilikuwa mchezaji mzuri tu nikicheza namba saba na tisa. Hata nilipokwenda Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya niliendelea kuwa mchezaji wa timu ya chuo.
Ndolanga anasema alipata ofa ya masomo kutoka Shirika la Chakula (FAO) kusoma hapo akichukua shahada ya uhifadhi viumbe, wanyama na mimea.
Anasema aliporejea nchini aliendelea na kazi Idara ya Wanyamapori, lakini wakati huo Serikali ilikuwa na utaratibu wa kuwachukua wasomi kuwapeleka vijijini kwa ajili ya kupeleka maendeleo.
Yeye alipelekwa Mbulu kuwa mkurugenzi wa maendeleo wa wilaya tangu mwaka 1972 hadi 1975 alipohamishiwa Arumeru na hapo ndipo safari yake ya kuongoza FAT ilipoanzia.
Anasema mwaka 1976 viongozi wa FA Arusha walishindwa kufanya vyema, hivyo mkuu wa mkoa wa Arusha wa wakati huo, Abdulnoor Suleiman alimwambia aende kunyoosha chama hicho ingawa wakati huo alikuwa ni meneja mkuu wa shirika la wanyamapori Arusha.
“Niliorganise mambo mbalimbali pale Arusha kisha nikawaacha waendelee, lakini baada ya muda walifanya uchaguzi nikagombea ili kuwa mjumbe wa mkutano mkuu FAT nikitokea Arusha nikashinda,” anasema.
Akiwa Arusha, FAT ilifanya mkutano mkuu Mbeya kuchagua viongozi na Said El Maamry alikuwa akigombea uenyekiti.
“Wakati huo, ili ugombee ilikuwa lazima upitishwe na  BMT,” anasema.
“El Maary alizuiwa na BMT, hivyo katika uchaguzi tukachagua makamu pekee. Nafasi ya  mwenyekiti nafasi yake haikujazwa. Uchaguzi uliofuata Mohammed Mussa akachaguliwa kuwa mwenyekiti na Meshack Maganga katibu wake.
“Hawa waliiongoza Stars kushiriki Kombe la Chalenji nchini Uganda mwaka 1992, baadaye kukawa na mkutano mkuu Mwanza, katika mkutano ule katibu alitoa taarifa ya kiwango cha timu kwenye Chalenji, akasema timu imecheza vizuri wakati tulifungwa mabao 5-0,” anasema.
“Akaulizwa swali kama tumefungwa 5-0 na unasema tumecheza vizuri, je tungewafunga wapinzani ungetoa sifa gani kwa Stars?, ilikuwa patashika mkutano ukataka kamati ya utendaji itoke nje kisha tukaamua iundwe kamati teule ya kusimamia FAT na kuuondoa madarakani uongozi uliokuwepo mwishoni mwa mwaka 1992.
Safari ya Ndolanga kuongoza FAT ikaanza mwaka 1993 ulipofanyika uchaguzi mkuu Kibaha, Pwani alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa FAT.
Anasema akiwa FAT aliongoza kwa misimamo hakutaka kuyumbishwa wala kumuonea au kupendelea klabu na kuikandamiza nyingine.
“Nilikuwa mwanachama wa Pan African lakini sikuwahi kuibeba Pan vivyo hivyo kwa klabu nyingine,” anasema Ndolanga.

Atoboa siri jina Tyson
Kila lilipotajwa jina lake liliambatanishwa na jina Tyson, bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Mike Tyson wa Marekani.
Kuna tetesi kwamba Ndolanga, ambaye pia alijulikana kama mbabe, aliwahi kumpiga waziri wakati akiwa mkurugenzi wa wanyamapori na kujipatia jina hilo.
“Kweli nilimpiga (alimtaja), lakini tukio hilo si chimbuko la jina la Tyson. Hili jina liliibuka baada ya kuishinda BMT mahakamani pale ndipo nikapewa jina la Tyson wa FAT wakimaanisha mbabe wa FAT,” anasema.
Anasema tukio la kumpiga waziri lilitokana na sababu ambazo alishindwa kujizuia.
“Unajua kuna falsafa imejengeka kuwa watu wa Musoma wana imani moja kwamba mwanamume asipompiga mke wake basi hawawapendi na wanaamini hakuna mwanamume ambaye anaweza kumtukana mwanaume mwingine kitakachotokea, lazima watapigana,” anasema.
“Na sisi Wamakonde tuna imani hiyo kwamba hakuna mwanamume anaweza kumtukana mwanaume mwingine. Lazima mpigane na atakayepigwa atamuamkia aliyempiga hadi anakufa. Ndicho kilitokea kwa kiongozi huyo ambaye anatokea mikoa ya kaskazini.”

Ajivunia hosteli TFF
Ingawa misimamo thabiti ndiyo inayokumbusha wengi enzi za Ndolanga, mwenyekiti huyo wa zamani wa FAT anasema hosteli zilizopo makao makuu ya TFF ndiyo alama kubwa ya uongozi wake.
“Tulizijenga mimi na Rage lakini kingine ni kuhakikisha waamuzi wanachezesha kwa weledi na kuweka mkazo klabu za Ligi kuu kuwa na timu za vijana,” anasema.
Pia Ndolanga anakumbuka tukio la Simba kukosa Kombe la CAF mwaka 1993 baada ya kufungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast, kama moja ya matukio ambayo hatasahau.
Lakini Ndolanga anasema jambo ambalo hakuweza kulifanya akiwa rais wa FAT ni kushiriki kubadili mfumo wa soka la Tanzania kutoka ridhaa na kuwa wa kulipwa.

Advertisement