Kiungo Ng'anzi apishana na Rooney Marekani

Monday February 24 2020

Mwanaspoti, Kiungo Ng'anzi, Rooney,Tanzania, USA, Michezo, Mwanasport

 

By ELIYA SOLOMON

KAMA sio bilionea Mel Morris kuona kuna umuhimu wa kumrudisha Wayne Rooney nchini England basi huenda Ally Ng’anzi angepata nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwa gwiji huyo ambaye msimu uliopita alitamba Marekani akiwa na DC United.
Tayari Ng’anzi ambaye ni mchezaji wa MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech, amerejea zake Marekani lakini safari hii sio Saint Paul Jijini, Minnesota ambako alikuwa akiichezea Minnesota United kwa mkopo na badala yake ni Washington, D.C. ambako ndio maskani ya chama lake jipya ambalo Rooney alikuwa akilichezea.
Ng’anzi amepishana na Rooney ambaye Agosti 6 mwaka jana alifikia makubaliano na Morris ambaye licha ya kuwa mmiliki wa klabu hiyo ya Daraja la Kwanza lakini pia ni mwenyekiti, ili straika huyo akawe kocha mchezaji akisaini mkataba wa miaka miwili.
Kama ambavyo ilikuwa wakati akitua kwa mkopo Minnesota United kwa kuanzia kikosi B cha timu hiyo ambacho ni Forward Madison ndivyo ambavyo itakuwa hata katika chama lake jipya la DC United, Ng’anzi ataanzia Loudoun United.
Mataifa ya wenzetu yametengeneza misingi kwa vikosi vyao B kushiriki madaraja ya chini kwa lengo ya kuwaweka fiti wachezaji wao kabla ya kuanza kutumika katika vikosi vyao vya kwanza ambavyo mara nyingi hushiriki Ligi Kuu au madaraja ya juu.
Mbali na Rooney ambaye amepishana na Ng’anzi hawa hapa mastaa wengine ambao chipukizi huyo wa Kitanzania atajifunza mengi kutoka kwao kutokana na makubwa ambayo wamekuwa wakifanya kwenye klabu hiyo.

PAUL ARRIOLA
Ukimu-ondoa Rooney ambaye aliifungia DC United mabao 11 msimu uliopita, Paul Arriola alikuwa kati ya wachezaji muhimu ambao msimu uliopita alikuwa akitegemewa na timu hiyo.
Faida aliyonayo Ng’anzi ni kuwa atakuwa akipata nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha timu hiyo hivyo itakuwa fursa ya kuchota ujuzi kutoka kwa mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akicheza timu ya taifa ya Marekani.
Arriola ambaye alizaliwa Februari 5, 1995 nchini humo, amekuwa akitumika katika kikosi hicho kama mshambuliaji wa pembeni (winga). Msimu uliopita aliifungia klabu hiyo mabao sita.

LUCAS RODRIGUEZ
Licha ya kuwa ni kiungo, Lucas Rodríguez ambaye ni Muargentina amekuwa na uwezo mzuri wa kufunga. Msimu uliopita aliifungia DC United mabao sita sawa na Arriola, wachezaji hao walishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa klabu hiyo wakiwa nyuma ya nyota wa zamani wa Manchester United, Rooney.
Hapa ni mahala pake, anacheza nafasi ambayo Ng’anzi amekuwa akicheza ya kiungo hivyo itakuwa sehemu sahihi kwake ya kuchota ujuzi kutoka kwa Muargentina huyo ili kuwa bora zaidi.
Mbali na kuwa kiungo, Rodriguez amekuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji, akiwa na klabu yake ya kwanza kuichezea soka la kulipwa Estudiantes ya nchini kwao Argentina alikuwa akicheza zaidi katika nafasi hiyo.

ULISES SEGURA
Ni raia wa Costa Rica, amekuwa akicheza kama kiungo, Ulises Segura  ameifungia  DC United mabao matatu katika michezo 33 ya Ligi Kuu Marekani huku akitengeneza nafasi mbili tu.
Ni moja ya viungo ambao wamekuwa wakitegemewa na kikosi hicho, hapa pia ni sehemu ambayo anawezakujifunza mengi kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Ng’anzi.

FREDERICK         BRILLANT
Licha ya kuwa ni beki wa kati, Frédéric Brillant alionyesha uwezo mkubwa msimu uliopita mbali na kupambana na washambuliaji hatari kwenye Ligi hiyo, aliweza pia kufunga mabao matatu.
Mfaransa huyu, anaweza kuwa darasa kwa Ng’anzi ambaye kama atafanya vizuri kwenye kikosi cha vijana basi huenda akapata nafasi ya kupigania ubingwa wa MLS akiwa na mastaa hawa.

EMMANUEL       
 BOATENG
Hakufunga bao msimu uliopita lakini katika michezo minne aliyocheza ilitosha kutabiriwa kuwa huu unaweza kuwa msimu wake, amejiunga na DC United, Emmanuel Boateng akitokea LA Galaxy ambako alikuwa akicheza kikosi kimoja na Zlatan Ibrahimovic.
Boateng ambaye ni Mghana aliichezea LA Galaxy kwa misimu minne mfululizo kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiunga na chama hilo la Washington, D.C mwaka jana.
Ni Muafrika pekee aliyepo katika kikosi cha kwanza.

Advertisement