Mwanamke ashikilia usajili wa winga Yanga

Muktasari:

Bestine Kazadi alizaliwa mwaka 1963 nchini Ubelgiji na baba yake Kazadi Tshishishi aliwahi kuwa Rais wa AS Vita

Yanga ilikuwa katika mazungumzo na AS Vita ya kumuwania winga teleza, Tuisila Kisinda ikitumia vyema mwanya wa kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa timu hiyo ya DR Congo, Jenerali Gabriel Amis Kumba
Hata hivyo sasa italazimika kufanya kazi ya ziada kumnasa winga huyo baada ya AS Vita kumpata rasmi Rais mpya ambaye ni mwanamama, Bestine Kazadi mwenye umri wa miaka 57.
Mwanamama huyo ameingia madarakani baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana jijini Kinshasa.
Kazadi ambaye ni mtoto wa zamani wa Rais wa AS Vita, ameibuka rasmi mshindi wa kiti cha Urais wa timu hiyo mbele ya Eugène Diomi baada ya kupata jumla ya kura 38 huku mpinzani wake akipata kura 32.
Katika uchaguzi huo ambao ulimfanya Kazadi kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Urais wa AS Vita, jumla ya kura 72 zilipigwa ambapo mbili ziliharibika.
Kabla ya kushika nafasi hiyo ya Urais, Bestine Kazadi amewahi kutumikia nyadhifa mbalimbali za kiserikali na amekuwa shabiki wa klabu hiyo kwa muda mrefu.
Kazadi ambaye ni mwanasheria, anamiliki kampuni ya sheria lakini pia ni mshauri wa Rais wa DR Congo, Felix Tshisekedi
Kisila amekuwa katika rada za Yanga lakini mchezaji mwingine wa klabu hiyo ambaye amekuwa akiwindwa ni kiungo Mukoko Tonombe.
Tonombe amekuwa akiwaniwa na Simba lakini pia Yanga nao wanatajwa kuwa kwenye mpango wa kumsajili ili kuimarisha safu yao ya kiungo.