Mwamnyeto hapa Simba SC imelamba dume au garasa

Sunday April 5 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Mwamnyeto hapa Simba SC, imelamba dume au garasa, Coastal Union, tegemeo Wawa na Nyon

 

By CHARLES ABEL

Simba inatajwa kumalizana na beki wa Coastal Union, Bakari ‘Nondo’ Mwamnyeto ikiwa ni mkakati wa kuimarisha safu yao ya ulinzi ka ajili ya msimu ujao kusaidiana na Erasto Nyoni na Paschal Wawa ambao umri wao umeenda.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya Simba vinathibitisha kwamba Mwamnyeto huenda ukawa usajili wa kwanza ndani ya msimu mpya kwani mambo mengi yanakwenda sawa na kinachosubiriwa ni muda tu.
Ingawa mchezaji huyo na meneja wake wamekuwa wakisisitiza muda bado wa kuzungumzia ishu hiyo, habari za uhakika ni kwamba jambo hilo ni la kweli na upo uwezekano mkubwa beki huyo akawa ni miongoni mwa wachezaji wa Simba msimu ujao.
Simba wanaamini mchezaji huyo ni miongoni mwa mabeki bora zaidi kwa sasa na ambaye anaweza kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu.
Siku zote usajili wa mchezaji huwa ni kama bahati nasibu kwamba zipo nyakati mchezaji aliyesajiliwa anaweza akafanya vizuri lakini pia wakati mwingine anaweza kushindwa kutamba na akachemsha.
Hivyo kwa kuangalia dhana hiyo, inawezekana Mwamnyeto anaweza akafanya vizuri na kuwa msaada mkubwa kwa Simba lakini inawezekana pia mambo yakaenda kinyume na kile ambacho wengi wanakitarajia kutoka kwa beki huyo wa Taifa Stars.
Mwamnyeto kama ilivyo kwa wachezaji wengine, ana umuhimu na faida zake ndani ya uwanja lakini pia ana mapungufu yake anayotakiwa kuyafanyia kazi ili aweze kutamba.
Ingawa uwepo wa mwamnyeto kiuhalisia unaonekana utakuwa na faida kubwa kwa Simba, ifuatayo ni tathmini ya jinsi Simba inavyoweza kunufaika na Mwamnyeto lakini pia inaonyesha udhaifu wa beki huyo ambao anatakiwa kuurekebisha ili awe mchezaji mkubwa na bora zaidi.

Kwa nini Simba imelamba dume?
Umri mdogo wa Mwamnyeto ni moja ya mambo ambayo yataisaidia Simba kwa sababu ina uhakika wa kumtumia mchezaji huyo kama mbadala wa muda mrefu wa mabeki wake wawili tegemeo Wawa na Nyoni.
Nyota huyo aliyeibukia kutoka katika kikosi cha timu ya vijana cha Coastal Union, kwa sasa ana umri wa miaka 24 hivyo ikiwa hatopata fursa ya kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa na akajitunza vizuri, Mwamnyeto anaweza kuitumikia Simba kwa takribani miaka 10.
Lakini nidhamu yake ya hali ya juu nje na ndani ya uwanja ni sifa nyingine inayoweza kuipa faida Simba kwani mchezaji huyo ana uwezo wa hali ya juu wa kufanyia kazi kwa ufasaha mbinu na maelekezo ya benchi la ufundi lakini hata katika maisha ya kawaida, Mwamnyeto sio mchezaji ambaye anatajwa kujihusisha na tabia za ovyo.
Kiufundi na mbinu ni mchezaji anayeweza kucheza vyema nafasi ya beki wa kati kutokana na sifa zake za kukaba, kuipanga vyema safu ya ulinzi, kucheza kwa bidii na uwezo wa hali ya juu wa kuokoa mashambulizi hasa mipira ya juu itokanayo na mipira ya kurusha, kona, faulo na krosi.
Anaweza pia kuwa msaada katika ufungaji wa mabao kwa kutumia mashambulizi ya mipira hiyo ya juu na hesabu zake nzuri katika kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani zinaweza kuibeba Simba.
Ni mchezaji asiye na hofu ya kucheza mechi za ushindani wala kukabiliana na wachezaji wenye majina makubwa, tabia ambayo inahitajika kwa mtu anayecheza nafasi ya beki.

Haya yanaweza kumwangusha
Kiasili Mwamnyeto sio mzungumzaji sana iwe ndani na nje ya uwanja. Hilo linaweza kumgharimu ndani ya kikosi cha Simba kwani ni tofauti na maisha ya Coastal Union kwa sababu anapaswa kuwa na sauti yenye mamlaka kwa wenzake vinginevyo wanaweza kufanya makosa ambayo yanayoweza kumuingiza matatani hata yeye mwenyewe na timu kiujumla.
Pia beki huyo ana changamoto ya kutokuwa na kasi, ambayo inaweza kumpa wakati mgumu pale anapokutana na washambuliaji wenye kasi, chenga na maamuzi ya haraka pindi wawapo na mpira.
Kasoro nyingine ya Mwamnyeto ambayo anatakiwa aifanyie kazi ni uwezo wa kuanzisha mashambulizi au kuwachezesha washambuliaji wake kuanzia nyuma.
Mahitaji ya mchezo wa soka kwa sasa yamekuwa ni makubwa na mabao yanapikwa hata kuanzia kwa safu ya ulinzi hivyo kwa Simba ambayo ina nafasi kubwa ya kushiriki mashindano ya kimataifa inalazimika kuwa na beki ambaye anaweza kuanzisha na kushiriki katika mashambulizi kama ilivyo kwa Nyoni na Wawa.
Suala la uzoefu pia linaweza kuwa changamoto kwa Mwamnyeto kwani bado hajacheza idadi kubwa ya mechi za kimataifa jambo ambalo linahitajika kwa mchezaji wa klabu kubwa kama Simba.

Wadau wanamzungumziaje?
Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema kuwa Mwamnyeto ni mchezaji ambaye ana nafasi kubwa ya kufika mbali kisoka.
“Ni mchezaji mwenye nidhamu, anajituma, msikivu na ana kiwango bora ambacho naamini kikiimarika, atacheza soka la kulipwa katika klabu kubwa nje ya nchi sio hapa nchini tu,” alisema Mgunda.
Kocha wa Boma FC, Muhibu Kanu alisema kuwa ikiwa Simba itamsajili Mwamnyeto basi itakuwa imelamba dume.

“Ni kijana ambaye amefanya vizuri katika timu ya taifa licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa lakini ndani ya klabu yake amekuwa na muendelezo mzuri ambao unatupa matumaini kwamba Tanzania tumepata beki wa daraja la juu kama atajitunza.
Nadhani ni usajili mzuri kwa Simba kama itampata kwa sababu ni mchezaji ambaye ana sifa zote za kucheza nafasi ya beki wa kati,” alisema Kanu.

Advertisement