Mwadui yashtuka, yajipanga upyaaa

Friday November 8 2019

 

By Saddam Sadick,Mwanza

KOCHA Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam ni kama amejishtukia baada ya kufubguika akidai licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo kwao wanachukulia kama sehemu ya soka, lakini akitamba timu yake itabadilika na kufanya vizuri kwenye zijazo mara baada ya mapumziko mafupi ya Ligi Kuu.
Mwadui inayoshikilia rekodi ya kuwa timu pekee iliyowanyoosha watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba mpaka sasa imekusanya pointi 11 na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo na ilikuwa na mwenendo mzuri kwenye mechi zake za awali, lakini tangu waifunge Simba wamepoteza dira kwa kukubali vichapo viwili mfululizo dhidi ya Lipuli na Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, Kocha Adam alisema licha ya matokeo waliyopata bado hayajamfurahisha na kufafanua timu itabadilika na kupata ushindi katika michezo inayofuata.
Alisema kwa kipindi hiki cha mapumziko mafupi, makosa yaliyoonekana kwa mechi mbili za mwisho atayafanyia kazi ili kuweza kufikia malengo yao ya kumaliza mashindano katika nafasi nzuri.
“Ni matokeo ya soka kwani vijana walipambana ila walishindwa kupata tulichohitaji, hivyo tutajipanga upya kuhakikisha mechi zilizobaki tunafanya vizuri,” alisema Adam.
Hata hivyo Kocha huyo alikiri Ligi kuwa ngumu huku akibainisha kuwa msimu huu mambo yamekuwa tofauti kwani haijalishi uko nyumbani au ugenini isipokuwa popote unapata matokeo.
“Ukiangalia timu nyingi zimepoteza mechi nyumbani na nyingine zimepata ugenini,yote ni kutokana na ushindani wa Ligi kwahiyo kikubwa ni kujipanga kimkakati,” alisema kocha huyo.

Advertisement