Mugalu hana shughuli ndogo, awala Mlandege

Saturday October 17 2020

 

By Charles Abel

Kasi ya mshambuliaji Chris Mugalu katika kufumania nyavu imeendelea tena baada ya kuifungia Simba, mabao mawili katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege iliyochezwa katik Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini.

Mugalu alifunga mabao hayo mawili katika ushindi wa mabao 3-1 ilioupata katika mchezo huo ambao Simba ilitawala kwa asilimia kubwa.

Ilimchukua Mugalu dakika nane tu  mara baada ya filimbi ya kuanza mchezo kupulizwa kuitanguliza Simba katika mchezo huo kwa kufunga bao la kwanza akiunganisha kona ya Ibrahim Ajibu.

Kona hiyo ilitokana na mpira uliotemwa na kipa Mohamed Abdallah wa Mlandege kufuatia shambulio lililofanywa na mshambuliaji huyo.

Mugalu tena alikuja kufumania nyavu kwa mara nyingine mnamo dakika ya 68, akimalizia kwa ustadi pasi ya Mzamiru Yassin.

Pasi hiyo ambayo kabla ya kutua kwa Mugalu ilimgonga mmoja wa mabeki wa Mlandege na kumfikia mshambuliaji huyo ambaye alimpiga chenga kipa Abdallah na kukwamisha mpira wavuni kwa mguu wake wa kulia.

Bao hilo ni la saba katika mechi sita ambazo Mugalu ameichezea Simba ambapo amefunga katika kila mchezo.

Alifunga bao moja katika kila mchezo kwenye mechi dhidi ya  Vital'O, Biashara United, Gwambina FC, JKT Tanzania na African Lyon na leo amefunga mawili.

Ukiondoa bao hilo la Mugalu, Simba ilipata bao lingine kupitia kwa beki wa kati Ibrahim Ame aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Luis Miquissone katika dakika ya 16 huku lile la Mlandege likipachikwa na Yahya Haji katika dakika ya 71.

Mara baada ya kufunga mabao hayo, Mugalu alisema kuwa mafanikio yake yanatokana na jitihada.

"Namshukuru Mungu lakini naamini juhudi za pamoja za kitimu ndio chachu ya hili," alisema Mugalu

Advertisement