Manyika ahofia ufiti wa makipa Yanga

Muktasari:

  • Makocha wamepata muda wa takribani wiki mbili kuziandaa timu zao kabla ya kurejea kwa ligi Juni 13

KOCHA wa Makipa wa Yanga, Peter Manyika, amesema muda waliopata kuwaandaa wachezaji ni mfupi ni mchache kwa ajili ya  mechi zilizosalia za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam.
Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kurejea Juni 13 wakati siku 14 baadaye kutakuwa na mechi za robo fainali za Kombe la Shirikisho la Azam ambazo zilisimama tangu mwezi Machi kama hatua za kupambana na virusi vya Corona.
Akizungumza na Mwanaspoti Manyika anasema, muda huo ni mchache kiufundi kuwajenga wachezaji na hasa ikizingatia muda mrefu walikuwa wenyewe bila usimamizi.
"Hakuna namna tena, ndio hivyo inabidi tukubaliane na hali halisi tu, kwa kuwa kila mmoja wetu anatambua janga la Corona ndilo limepelekea yote haya lakini tunamshukuru Mungu michezo imerejea," alisema Manyika.
Anasema kwa muda mchache ambao wameanza mazoezi na kuwatizama vijana wake aliokuwa akiwaamini huko majumbani walikokuwa ameona kuna kazi ya ziada inahitajika kuifanya kabla ya kuanza kwa ligi.
Anasisitiza kuwa mazoezi ya mlinda mlango ni tofauti na mchezaji wa ndani hivyo inahitajika umakini mkubwa mchezaji akiwa katika mazoezi ya peke yake.
Yanga ilianza mazoezi Jumanne ya wiki iliyopita katika viwanja vya Chuo cha Sheria vilivyopo Jijini Dar es Salaam na kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo wachezaji wote walipimwa afya zao huku mazoezi yakifanyika kwa taadhari kubwa ya maambukizi ya virusi vya Corona.