Mambo ya Singano TP Mazembe si mchezo

Monday July 15 2019

 

By Doris Maliyaga

MAMBO ya mshambuliaji mpya wa TP Mazembe, Ramadhani Singano ‘Messi’ si mchezo kwani saini yake imemfanya alipwe kiasi cha Dola 4000 (Sh.9 mil) kila mwezi ya mshahara, huku usajili wake ni Dola 50,000 (Sh125 mil).

Wakala wa mchezaji huyo, Rashid Ally alisema Singano amesaini mkataba wa miaka minne na TP Mazembe baada ya Moise Katumbi kuona video zake akasisitiza lazima atue kwake na safari yake ilikuwa ni pamoja na Mrisho Ngassa, lakini ameshindwa kwenda baada ya Yanga kumwekea pesa mezani kabla ya safari, akasaini.

“Safari ilikuwa aende kwanza Katanga, lakini Don Bosco wakampenda. Baadaye Kocha wa Don Bosco alikamwonyesha Katumbi zile video ndio akamwambia huyu ni wakucheza TP Mazembe. Ilikuwa aende na Ngassa lakini ndio hivyo, mambo hayakwenda sawa,” alisema jamaa huyo.

Alisema TP Mazembe ni klabu kubwa Afrika upo uwezekano wa Singano akawa na maisha mazuri zaidi katika timu hiyo endapo ataonyesha kiwango cha juu.

Singano alisaini mkataba huo juzi jioni katika ofisi za tajiri wa DR Congo, Moise Katumbi jijini Lubumbashi baada ya kuachwa huru na Azam FC na atakuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi hicho kuanzia msimu ujao na atakuwa pamoja na Mtanzania mwingine Eliud Ambokile.

Mshambuliaji huyo aliondoka nchini juzi Jumanne kwa Ndege ya Shirika la Kenya akipitia Nairobi.
Pia, awali alikuwa asajiliwe Ibrahim Ajibu ambaye alikataa na kujiunga na Simba akitokea Yanga. Singano anakuwa mchezaji wa pili Mtanzania kusajiliwa na TP Mazembe msimu huu baada ya Ambokile. Awali wachezaji, Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa JS Saoura ya Algeria na Ngawina Ngawina walicheza hapo.

Advertisement

Advertisement