Lukaku amfuta kabisa Solskjaer hadi aibu

Muktasari:

Lukaku alisema hajawahi kuwa na matatizo na makocha waliomnoa, lakini alipoulizwa nani alikuwa vizuri chini yake, Solskjaer hakutajwa kabisa na mshambuliaji huyo kwenye orodha ya makocha wake.

MILAN, ITALIA . STRAIKA, Romelu Lukaku amemfuta kabisa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer kuwa ni moja ya makocha waliowahi kumnoa kwa mafanikio.
Staa huyo wa Kibelgiji aliondoka Man United kwenda Inter Milan kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi na tangu atue huko kwenye Serie A amekuwa moto si mchezo. Chini ya Solskjaer, Lukaku alijikuta akipoteza nafasi yake ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Man United baada ya Jose Mourinho kuondoka na kocha huyo mpya kutua Old Trafford.
Lukaku alisema hajawahi kuwa na matatizo na makocha waliomnoa, lakini alipoulizwa nani alikuwa vizuri chini yake, Solskjaer hakutajwa kabisa na mshambuliaji huyo kwenye orodha ya makocha wake.
Lukaku alisema: "Nadhani ni Roberto Martinez, Ronald Koeman na sasa Antonio Conte. Nadhani pia Jose Mourinho kama angepata wachezaji aliowataka, nadhani angefanya vizuri kuliko tulivyofanya. Kuna Steve Clarke, namtaka maalumu alinipa nafasi ya kucheza Ligi Kuu England nikiwa na miaka 19. Na bila shaka kocha wangu wa kwanza huko Anderlecht, Ariel Jacobs, ambaye alinipa nafasi nikiwa na miaka 16. Hao ndio makocha ambao daima nitawaheshimu."
Lukaku amekiri kwamba alifahamu wazi kwamba anapaswa kuachana na Manchester United baada ya kuwa na msimu wa hovyo ikiwa ni miaka miwili tu tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Everton.
"Uamuzi wangu niliufanya Machi, nilikwenda ofisini kwa kocha na kumwambia kwamba muda wangu wakuwa hapo imefika mwisho, hivyo natafuta mambo mengine," alisema.
"Nikiwa kwenye kiwango na sikuwa nachezeshwa. Niliona ni vyema kwa pande zote mbili tukaachana tu. Nadhani nilifanya uamuzi sahihi. Man United yenyewe ilitoa nafasi kwa wachezaji makinda hivyo nilidhani ilihitajika kufanya hivyo."