Kocha Ndanda aifagilia Simba, hesabu kali FA Cup

Monday June 29 2020Kocha wa Ndanda FC, Meja Mstaafu Abdul Mingange

Kocha wa Ndanda FC, Meja Mstaafu Abdul Mingange 

By Olipa Assa

Siku moja baada ya Simba kujihakikishia taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kocha wa Ndanda FC, Meja Mstaafu Abdul Mingange amewamwagia sifa na kukiri walistahili kuwa mabingwa
Mingange amesema Simba haijabahatisha kutwaa ubingwa huo,bali ilikuwa na vitu vilivyochangia mafanikio hayo kama uongozi imara,makocha wenye uwezo, wachezaji bora na uwanja wao wa mazoezi.
"Simba imestahili kutawazwa Mabingwa,wapo vizuri kuliko timu nyingine ambazo zinacheza Ligi Kuu Bara,ndio maana nimetaja vitu ambavyo vimewafikisha katika mafanikio hayo hawakubahatisha wala kupendelewa.
Mimi ni kocha sitaki kuongea propaganda  za mashabiki, uwazi wangu utufunze kujipanga katika mambo muhimu yanayotakiwa katika soka, lengo tuwe na ushindani unaotakiwa ambao bingwa akipatikana anakuwa anafika mbali katika michuano ya kimataifa,"amesema.
Kuhusu uwezekano wa kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Mingange alisema kuwa wanaweza kufanya vizuri ikiwa watajiandaa vyema.
"Licha ya kwamba mwaka huu waliishia hatua za awali katika michuano ya CAF haina maana kwamba hawakuwa katika uwezo, isipokuwa naona wamepata funzo la kuweka umakini kwa kila mechi,"amesema Mingange.
Katika hatua nyingine, Mingange alisema anaiandaa vyema timu yake kuhakikisha inapata ushindi dhidi ya Sahare All Stars katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam keshokutwa.
"Timu za madaraja ya chini zikikutana na za ligi kuu huwa zinakamia, hivyo tumejipanga kwa namna yoyote kukabiliana na hilo,kwani natambua imetusoma wakati tunacheza mechi za ligi kuu.
Awamu hii tunapambana kadri tuwezavyo kuhakikisha tunavuka hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA,baada ya kuishia robo fainali huko nyuma,"alisema Meja Mingange.
Alisema anaamini Sahare All Stars itawapa ushindani mkubwa kwani kundi kubwa la wachezaji wao linataka kutumia fursa hiyo kujitafutia soko.
"Ukiachana na hilo kuna wachezaji ambao watataka kuonekana na Ndanda FC ili kupata bahati ya kucheza ligi kuu kwani naamini hatushuki,"alisema.

Advertisement