Kikapu walia na Corona

Muktasari:

"Pia ratiba ya ligi  za mikoa nazo vimevurugika, kulikuwa na michuano ya Kombe la Muungano na ile ya kimataifa nayo haitakuwepo tena. Kubwa zaidi tulikuwa na mkutano wa kubadirisha Katiba uliokuwa ufanyike kesho Jumamosi, Aprili 4 nao hautakuwepo." amesema Magesa

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), Phares Magesa amesema kuwa janga la mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiutendaji katika shirikisho hilo.

Magesa amesema moja ya athari ambazo wamekumbana nazo kama shirikisho ni kusimama kwa michuano ambayo ilikuwa inakaribia kuanza hivi karibuni, pamoja na kuathiri uchumi wa wahusika wa mchezo huo.

''Unajua janga hili limeathiri sana mchezo huu, kwani kulikuwa na michunao ya vijana 'Junior NBA' ambayo ilikuwa ianze hivi karibuni lakini imeshindikana kuanza kwa sababu ya janga hili.

"Pia ratiba ya ligi  za mikoa nazo vimevurugika, kulikuwa na michuano ya Kombe la Muungano na ile ya kimataifa nayo haitakuwepo tena. Kubwa zaidi tulikuwa na mkutano wa kubadirisha Katiba uliokuwa ufanyike kesho Jumamosi, Aprili 4 nao hautakuwepo." amesema Magesa

Mbali na hilo Magesa amesema kuwa mlipuko wa virusi hivyo unachangia sana kushuka kiuchumi kuanzia kwa klabu na hata wachezaji wenyewe, maana kwa sasa hakuna mapato yeyote yanayopatikana kwenye mchezo huo.

''Janga hili lina athari kubwa sana kwenye uchumi, kuanzia klabu na hata wachezaji, kwa sasa wanapitia nyakati ngumu sana, maana hakuna chochote wanachoingiza, kwa sababu mchezo wenyewe hauchezwi hivyo hata kama kulikuwa na wadhamini nao hawawezi kutoa pesa zao sehemu ambayo hawatangazwi"

Magesa amesisitiza kutofanya shughuli zozote zinzohusiana na mchezo huo mpaka pale Serikali na mamlaka za juu za mchezo huo zitakapotoa tamko.
 
"Hatuwezi kusema kuwa tutaanza shughuli zetu baada ya muda gani, tunachosubiri ni tamko la Serikali ikiwa wataruhusu tena michezo kuanza, kabla ya hapo tulipokea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Afrika (FIBA) kututaka kusitisha shughuli zote za mchezo huu, kutokana na  hali hii," amesema Magesa