Kelvin wa Serengeti Boys atimkia Denmark kujifua

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo pamoja na wakala wake waliondoka jana jioni kuelekea nchini Denmark kwa majaribio yatakayodumu kwa siku 18 katika timu ya HB Koge.

 Mwanza. Mshambuliaji tegemeo wa Serengeti Boys, Kelvin John amekwenda nchini Denmark kwa ajili ya kufanya majaribio katika klabu ya Hb Koge inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Mshambuliaji huyo aling’ara katika mashindano ya kuwania kufuzu AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 yaliyofanyika mwezi Julai hapa nchini na kuibuka mchezaji Bora.
John alisafiri jana jioni kuelekea nchini humo ambapo pamoja na kufanya majaribio Klabuni hapo atakuwa na program maalumu ya maendeleo itakayodumu kwa siku 18.
Skauti na wakala wa kituo cha michezo cha Baras Sports Management cha wilayani Magu mkoani hapa, Jamari Barass alisema nafasi hiyo ni muhimu kwa nyota huyo na timu nzima ya Serengeti Boys.
Alisema kuwa wao kama kituo cha Barass Sports Management kinaona fahari kupewa majukumu ya kumsimamia na kumwendeleza kijana huyo kipaji chake.
“Hii ni nafasi nzuri na muhimu kwa John (Kelvin) pamoja na timu yetu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti Boys, lakini hata sisi kampuni ya Barass tunafurahi kupewa majukumu ya kusimamia tunaamini ataipeperusha Bendera ya Taifa”alisema Barass.
Naye Kelvin John alisema anashukuru kwa nafasi hiyo aliyopata nje ya nchi na kuahidi anaenda kupambana na matarajio yake ni kufuzu.
“Nashukuru kupata nafasi hii, lakini niwaambie Watanzania naenda kupambana na kufanya vizuri, niwaombe waendelee kuniombea niweze kuipeperusha vyema Bendera ya Taifa letu,” alisema Kinda huyo.