Katwila anasubiri kipyenga tu aliamshe

Friday August 9 2019

 

By Olipa Assa

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema maandalizi yao hayana presha, akidai timu yake kukaa kwa pamoja kwa muda mrefu kunawapa kujiamini na kuona kila kitu kwenye ligi ni cha kawaida na wanasubiri msimu uanze wafanye mambo.
Katwila amesema anakiamini kikosi chake kwamba kitafanya kazi nzuri na kuwapa changamoto wapinzani wao ambao wana wachezaji kibao wa kigeni.
Amesema anajivunia kuwa na wachezaji wazawa ambao wanalibeba soka halisi la Tanzania na kwamba misimu mingi wamekuwa mwiba dhidi ya timu ambazo zimejaza mapro.
"Sisi tupo tayari ligi ianze muda wowote kuanzia sasa kwani, hakuna kipya ambacho tunakisubiri ama hakuna maandalizi ya ajabu kwani kama ni ligi tumezoea kuicheza na kikosi hakijavurugika sana.
"Tumecheza na KMKM mara mbili ya kwanza tuliwafunga Jamhuri bao 4-1, nyingine tumechezea Manungu tumewafunga bao 1-0, tulitaka kucheza na Dynamo lakini mwisho wa siku ratiba yetu ilikuwa imebana, lakini kila kitu kinakwenda sawa,"anasema.

Advertisement