Huyu Jesca kawa mtamu balaa

NYOTA njema huonekana asubuhi. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Jesca Ngisaise ambaye ameweka rekodi kabambe kwenye mpira wa kikapu hapa nchini.

Jesca mwenye umri wa miaka 17 ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga pointi nyingi katika mchezo mmoja na hakuna mwingine aliyewahi kufanya hivyo nchini iwe kwa wanaume au wanawake katika historia ya mchezo huo.

Mchezaji huyo mrefu kiasi alifunga pointi 105 timu yake ya JKT Stars ilipoichapa Ukonga Princess pointi 166-7 katika mechi ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), iliyofanyika Agosti 22, mwaka huu.

Achana na rekodi hiyo, pia ndiye anayeongoza kwa kufunga pointi nyingi ligi ya RBA upande wa wanawake akifunga pointi 229, akifuatiwa na Faraja Malaki wa Jeshi Stars mwenye nazo 105.

Vilevile ndiye mchezaji anayeongoza kufunga kwa mitupo mitatu (three points) akifunga mara 28, akifuatiwa na Faraja aliyefunga mara tisa.

Pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya wanawake na aliwahi kwenda Afrika Kusini 2017 alikoshiriki mafunzo ya mchezo huo yaliyoendeshwa na makocha wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), maarufu Basketball Without Borders.

Mchezaji huyo aliyeichezea timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 16, aliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Afrika Mashariki huko Kenya mwaka 2017 na kuchaguliwa kuiwakilisha nchi kwenye mafunzo hayo. Kutokana na uwezo aliouonyesha katika kambi hiyo, Jesica alichaguliwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliounda timu ya nyota bora wa Afrika na kucheza mechi ya utangulizi kabla ya mchezo wa NBA Africa uliofanyika Sun Arena, Pretoria mwaka 2018.

KUWEKA REKODI

Jesca anasema anafurahi kuwa mchezaji wa kwanza kuweka rekodi ya kufunga pointi nyingi katika mchezo mmoja kwenye historia ya mpira wa kikapu nchini. “Nimejisikia vizuri. Ni jambo zuri na la kujivunia sana,” anasema.

“Watu wanaweza kuona ni rahisi wakidhani tulikutana na timu chovu, lakini kufunga pia ni kipaji, maandalizi na kutuliza akili, na ndicho nilichokifanya siku ile kuhakikisha nafasi niliyoipata naitumia vizuri.

“Nitaendelea kujibidisha ili kuweka rekodi nyingi zaidi kwani malengo yangu sio kucheza hapa tu nataka nicheze nje ya nchi kwenye ligi kubwa.”

AMIMINIWA SIFA

Kamisaa mzoefu wa kikapu, Hamidu Alekwa anamsifu Jesca kuwa na kipaji kikubwa na kama akijituma anaweza kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kucheza ligi kubwa nje ya nchi.

“Sio jambo rahisi kufunga pointi 105 katika mchezo mmoja. Tangu nacheza mpaka nimekuwa kamisaa kwa miaka mingi na sasa nazeeka hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo hapa nchini,” anasema.

“Ni mchezaji anayejituma uwanjani, mwenye kipaji na mtulivu pale anapofika katika eneo la kufunga.Hana papara, kama akiendelea hivyo basi anaweza kutoka na kucheza ligi kubwa nje ya nchi.”

VIONGOZI waAMKe

Kwa upande wake, Jesca anasema licha ya mpira wa kikapu kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji, lakini haupewi kipaumbele na uongozi jambo linalosababisha kushusha morali ya wachezaji wengi hasa wanawake.

“Kikapu kwa upande wa wanawake hawakipi sana kipaumbele kama ilivyo kwa wanaume, na kama ilivyo kwa nchi nyingine za wenzetu,” anasema.

“Nafikiri tatizo lipo kwa viongozi wenyewe kwani kama uongozi ukiwa mzuri kila kitu kitaenda sawa. Viongozi wanatakiwa kuamka na kuupa mchezo huu kipaumbele na baada ya hapo wachezaji kujitoa.”

Jesca anasema nchi mbalimbali za Afrika zimeupa kipaumbele kikubwa mchezo huo tofauti na hapa nchini unaoangaliwa zaidi ni soka. “Nimeshasafiri mara tatu nchi kadhaa kama Afrika Kusini, Senegal, Kenya, Rwanda - nilikuwa nachanguliwa kuiwakilisha nchi katika mafunzo ya vipaji wakati nachezea Ukonga Queens na nimeona jinsi wenzetu wanavyouthamini huu mchezo.

“Yaani kule miundombinu sio sawa na kwetu. Hapa viwanja tunavyochezea sio rafiki kabisa. Tunacheza basi tu tutafanyaje na kwa sababu tunaupenda mchezo huu,” anasema Jesca

“Sisi kama wachezaji tunajitoa, lakini kuanzia mwanzo wa ligi mpaka mwisho hakuna tunachopata ukilinganisha na nchi za wenzetu au ukilinganisha na mchezo wa soka ambao wenzetu wanapewa kipaumbele.

“Jambo hili linakatisha tamaa kwani linasababisha watu wengi wenye vipaji kushindwa kujitokeza kuonyesha vipaji kwa sababu hakuna wanachopata.”

Jesca ameiomba Serikali kuupa kipaumbele mchezo wa mpira wa kikapu huku akiwataka wadhamini kujitokeza kudhamini ili kuwapa chachu wachezaji wengi wenye vipaji kujitokeza kucheza.

“Ninachoiomba Serikali na viongozi wa michezo waupe kipaumbele mchezo wetu kama wenzetu wanavyoupa kipaumbele mchezo huu nchini mwao,” anasema.

“Katika nchi nyingine mfano Rwanda mchezo wa mpira wa kikapu umekuwa kama mchezo wao wa Taifa tofauti na sisi hapa ni soka soka soka tu.

“Sisi tunaweza kikapu na tunacheza vizuri kwani hata ukiangalia kwenye ligi inayoendelea kuna wachezaji wengi wana vipaji hata wakisema leo wachague wachezaji watakaoenda kuiwakilisha nchi kimataifa wapo wengi na wataenda kutikisa.”

“Sasa hivi hakuna udhamini - yaani tunacheza ligi bure hatupati chochote ni kama kujifurahisha tu.

“Kuna kipindi kulikuwa na wadhamini, lakini waliondoka sijui nini tatizo, hivyo viongozi ndio wanajua na wanatakiwa kujitafakari ili kuukoa huu mchezo.”

viWANJA

Jessica anasema tatizo lingine linalosababisha mchezo wa kikapu kutoendelea ni ukosefu wa viwanja bora.

Anasema kama lisipotafutiwa ufumbuzi haraka, basi vipaji vingi vya mchezo huo vitapotea kwa kuwa wachezaji wengi wako mitaani, lakini wanakosa pa kuvionyesha.

“Nakumbuka 2014 wakati ndio naanza kujifunza mpira wa kikapu na naichezea Ukonga Queens nikiwa Sekondari ya Juhudi iliyopo Ukonga haikuwa na uwanja, tulikuwa tunatoka shule tunaenda kutafuta sehemu ya kiwanja, tunaomba tunafanya mazoezi huku tunashiriki ligi lakini tulikuwa tunajitahidi hadi tunafika fainali,” anasema Jesca.

Jesca ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto saba, alianza kucheza mchezo huo 2014 katika timu ya Ukonga Queens kabla ya JKT Stars kumsajili mwaka huu, ambao wamemuahidi kumpeleka mafunzoni na kumpatia ajira endapo ikitokea.

“Najisikia vizuri kutoka Ukonga Queens.”