Huko Namungo kuna majanga

Saturday August 17 2019

 

By Yohana Challe

IKIWA imebaki wiki moja tu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu mpya wa 2019-2020, huko Namungo FC kumeanza majanga baada ya baadhi ya nyota wake kupata pacha kwa kuwa majeruhi.
Mmoja ya nyota walianza kuipa wasiwasi Namungo iliyopanda Ligi Kuu kutoka Daraja la Kwanza (FDL) ni mchezaji wa kulipwa kutoka Ivory Coast, Toure Sie Leopold aliyeumia majuzi kwenye mechi ya kirafiki na kuwatia hofu makocha wake.
Kocha wa Makipa, Emmanuel Kingu alisema mchezaji huyo ameachwa Dar es Salaam kwa matibabu wakati wachezaji wengine wakiwa wamerudi Lindi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
"Sijajua kama atawahi michezo ya awali ya ligi au atakuwa nje kwa muda gani, tunasubiri  ripoti ya daktari itakavyoeleza ndipo tutakapojua cha kufanya katika kukiimarisha kikosi chetu, ila ni moja ya wachezaji walio majeruhi," alisema Kingu.
Namungo  juzi Alhamisi ilicheza mchezo wa kirafiki na Azam FC na kukubali kichapo cha mabao 8-1 ikiwa ni kati ya mechi za kutesti mitambo ambayo, makocha wameutumia kubaini udhaifu katika kikosi chao na sasa wanaenda kurekebisha kabla ya ligi kuanza Agosti 24.

Advertisement