Huko FDL kuna mtu atalizwa mjue

ULE uhondo wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) unatarajia kuendelea kesho Jumamosi, huku Dodoma FC ikihamishia mchezo wake kwenye Uwanja wa CCM Gairo ikiwa siku chache baada ya Mtibwa kutangaza kuutumia uwanja huo kwenye michezo yake ya Ligi Kuu.
Mabadiliko ya uwanja, yamesababishwa na muingiliano wa ratiba katika uwanja wa CCM Jamhuri ambapo uwanja huo kwa sasa una matumizi mengine ya kijamii.
Pamoja na mabadiliko hayo, uongozi unawaomba mashabiki wa timu wasiache kujitokeza kwa wingi Mjini Gairo ili kuwaongezea morali wachezaji kwenye mchezo huo muhimu, huku kwingineko mashabiki wakitarajia kupata uhondo kwenye viwanja tofauti katika vita ya pointi tatu.
Kundi A, Ihefu FC atacheza na Pan African, Boma FC na African Lyon, Dodoma FC dhidya Mlale FC, Njombe Mji na Majimaji FC, Friends Rangers atakipiga na Iringa United wakati Reha atacheza na Mbeya Kwanza.
Kundi B' maafande wa Transit Camp hali yao ni tete na inaendelea kushika nafasi ya mwisho ikiwa na sare mbili pekee huku michezo mingine ikichezea vichapo na kesho itakipiga na Gwambina FC itakayokuwa nyumbani.