Hatima Manchester City, UEFA mwezi ujao

Wednesday May 20 2020

 

Manchester, England. Rufaa ya Manchester City ya kupinga adhabu ya kufungiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili ijayo itatolewa uamuzi mwezi ujao na mahakama ya kimataifa ya usuluhisi wa michezo duniani (Cas).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari, rufaa hiyo itasikilizwa kuanzia Juni 8 hadi 10 na baada ya hapo itatolewa uamuzi.
Manchester City walikata rufaa hiyo kupinga uamuzi wa kuwazuia kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili mfululizo na faini ya Pauni 25 milioni kwa kosa la kuvunja kanuni za matumizi ya fedha
Timu hiyo ilidaiwa kulidanganya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) juu ya matumizi yake ya fedha kinyume na kanuni zilizowekwa za usawa wa matumizi (Financial Fair Play)
Awali rufaa hiyo ilikuwa isikilizwe na kutolewa uamuzi mwezi Mei lakini kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, duniani ilishindwa kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo unasubiriwa kwa hamu kwani ndio unaweza kutoa muelekeo mpya wa uwakilishi wa timu za England katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ikiwa adhabu hiyo kwa City itaendelea au kuongezwa, maana yake timu itakayoshika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi itapata fursa ya kushiriki mashindano hayo.
Lakini pia unaweza kuamua hatima ya kocha Pep Guardiola na baadhi ya mastaa klabuni  kama wataendelea kubakia au la.
Miongoni mwa nyota hao ni kiungo Kevin De Bruyne ambaye amefichua kuwa uamuzi wa rufaa hiyo utaamua kwa kiasi kikubwa uelekeo wake.
"Naendelea kusubiri.Naiamini timu yangu.Pale uamuzi utakapotolewa nitafanya nitapitia kila kitu. Miaka miwili itakuwa mingi mno. Ingekuwa ni kesi ya mwezi mmoja ningeangalia. Inabakia kuwa changamoto ya kuwa bora na nahitaji hilo. Kinachokuja kinakuja," alisema De Bruyne.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, City inasubiria mchezo wa marudiano nyumbani wa hatua ya 16 Bora dhidi ya Real Madrid baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini katika mechi ya kwanza.

Advertisement