Coutinho anataka kurudi Liverpool

Saturday July 13 2019

 

BARCELONA, HISPANIA.KIUNGO fundi wa mpira Barcelona, Philippe Coutinho amefungua milango wazi ya kurudi kwenye klabu yake ya zamani Liverpool kama itamfuata na kutaka huduma yake katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mbrazili huyo ameweka wazi mpango wake wa kuachana na maisha ya Camp Nou baada ya kushindwa kufanya kweli kwa kipindi cha miezi 18 aliyodumu kwenye timu hiyo.
Coutinho aliigharimu Barcelona Pauni 142 milioni kutoka Anfield Januari mwaka jana na mabingwa hao wa La Liga wanataka tu kumuuza haraka iwezekanavyo ili kurudisha pesa yao.
Kocha Jurgen Klopp ameambiwa aende kuinasa huduma ya kiungo huyo na kumrudisha Anfield kama kweli anataka kikosi chake kiwe na nguvu ya ziada na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2019/20.
Kinachoelezwa ni kwamba Liverpool itamsajili Coutinho kwa bei ya chini, lakini saini yake haitapatikana kirahisi kutokana na Paris Saint-Germain nayo kumhitaji.
Taarifa za kutoka Nou Camp zinadai Coutinho safari inamhusu baada ya Antoine Griezmann kudaiwa atakapotua kwenye timu hiyo atakabidhiwa jezi namba 7 ambayo imekuwa ikivaliwa na Mbrazili huyo.
Barcelona imedaiwa iko kwenye hatua za mwisho kabisa za kumnasa Griezmann ikipanga kulipa Pauni 107 milioni ili kuvunja mkataba wake na Atletico Madrid na jambo hilo linaweza kuwa limefanikiwa hadi itakapofika keshokutwa Jumatatu.
Jezi namba saba huko nyuma kwenye kikosi cha Barcelona iliwahi kuvaliwa na mastaa kama Laszlo Kubala, Pep Guardiola, Luis Figo na David Villa.
Taarifa nyingine zinadai kiungo mpya, Frenkie de Jong atavaa jezi namba 21, ambayo kwa sasa ilikuwa ikishikiliwa na Carles Alena.

Advertisement