Corona yaleta majanga Kenya, mashabiki wazuiwa viwanjani

Muktasari:

Baadhi ya Ligi zilizositishwa mara moja ni  mashindano ya mashinani ya FKF na ligi kuu ya wanawawake (KWPL), Ligi ya daraja la kwanza la wanawake, Mechi zote za matawi za FKF, Ligi ya taifa ya daraja la kwanza na pili na mashindano yote ya kuibua vipaji.

MASHABIKI wa soka nchini Kenya, hawataruhusiwa kuingia uwanjani kutizama mechi zote za raundi ya 24 za Ligi kuu ya Kenya (KPL), zitakazopigwa wikendi hii, huku michezo mingine ikisitishwa mara moja, kutokana na hofu ya Virusi vya Corona vilivyoingia nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Kenya(FKF), iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Barry Otieno, Ligi nyingine ambayo mechi zake zitaendelea wikendi, bila ya mashabiki ni National Super League na FKF Cup.
Hata hivyo, kuanzia Jumatatu (Machi 16) KPL, NSL na FKF Cup zitaungana na michezo mingine iliyositishwa katika harakati za kupunguza madhara ya maambukizi ya kirusi cha Corona, ambayo imethibitika kuingia nchini.
Baadhi ya Ligi zilizositishwa mara moja ni  mashindano ya mashinani ya FKF na ligi kuu ya wanawawake (KWPL), Ligi ya daraja la kwanza la wanawake, Mechi zote za matawi za FKF, Ligi ya taifa ya daraja la kwanza na pili na mashindano yote ya kuibua vipaji.
Aidha, katika kuhakikisha wachezaji wanakuwa salama, wakati wa mechi hizo za wikendi, FKF ilisema, hakutakuwa na utamaduni wa kusalimiana kwa mikono, kabla na baada ya mechi hizo kufanyika.
Uamuzi wa FKF umekuja saa chache baada Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, kutangaza Corona kuingia nchini, baada ya mwananchi mmoja aliyeingia akitokea Marekani kubainika kuambukizwa viruzi hivyo vilivyosababisha vifo vya watu 3000 mpaka sasa.
Katika kuitikia wito wa Serikali ambayo imepiga marufuku mikusanyiko ya watu, shirikisho kadhaa pia zimeshatangaza kuahirisha na kufuta ratiba za michezo ambayo ilikuwa ifanyike katika kipindi hiki hadi pale usalama wa kiafya utakapokuwa sawa.
Shirikisho la Raga (KRU), ilikuwa ya kwanza kuchukua hatua, baada ya Alhamisi hii kufuta mechi ya Repechage Cup, kati ya timu ya taifa ya wanawake Lionesses dhidi ya Colombia, iliyopaswa kufanyika Aprili 8, Jijini Nairobi kutokana na hofu ya COVID-19.
Siku moja baadae, KRU tena ikasitisha mashindano yake yote ya msimu huu wa 2019/20. Kwa mujibu wa taarifa ya KRU, Ratiba zote za Kenya Cup, Eric Shirley na nusu fainali ya mashindano ya KRU ambayo iliratibiwa kufanyika kesho, zitasimama kwa kuda usiojulikana.
Ikumbukwe pia mashindano ya Gofu ya Magical Kenya Open, yaliyotarajiwa kufanyika Machi 12-15, ndiyo yalikuwa ya kwanza kuathiriwa na hofu ya maambukizi ya Coronavirus ambayo imeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 3000. Kenya Open imeahirishwa kwa siku 30.
Shirikisho la mchezo wa Magongo (KHU), nalo limetangaza kusitisha mechi zote za ligi ya mchezo huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mratibu msaidizi wa ratiba za KHU, Moses Majiwa. Shirikisho la Voliboli nchini (KVF), nalo halijaachwa nyuma.
Katika taarifa yake ya dharura kwenda kwa viongozi wote wa matawi wa KVF, Waithaka Kioni ambaye ni Rais wa KVF, alisema kama mashindano ya voliboli yanayoendelea katika ngazi ya kitaifa na mashinani yamesitishwa mara moja hadi pale itakapotangazwa tena.
Machi 12, Shirikisho la Riadha nchini (AK), ilisema imelazimika kuwazuia wanariadha wote kutotoka nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya tahadhari, ambayo ilikuja siku moja baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kutangaza kirusi cha Corona kuwa tishio namba moja duniani.