Bodaboda ya Mwanaspoti yaenda TMK

Friday July 12 2019

 

By Charles Abel

MKAZI wa Temeke, Gizirary Malibiche ameibuka mshindi wa Bodaboda katika droo ya kwanza ya Promosheni ya gazeti hili iliyofanyika Tabata jijini Dar es Salaam  leo Ijumaa.
Promosheni hiyo ilizinduliwa rasmi Julai Mosi, ikiwahusisha wasomaji wa gazeti hili ambapo kila wiki, kutakuwa na washindi wa zawadi ya Bodaboda, simu ya mkononi na fedha taslimu kiasi cha Sh 100,000.
Malibiche ambaye ni mkazi wa Tandika, aliungana na washindi wengine sita ambao mmoja alishinda zawadi ya simu ya mkononi huku wengine watano wakishinda fedha taslimu.
Aliyeibuka mshindi wa zawadi ya simu ya mkononi katika droo ya promosheni hiyo na kurushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha Azam, ni Daud Charles mkazi wa Mbezi Mpiji Magohe.
Mbali ya wawili hao, washindi wengine watano ambao kila mmoja alinasa mchongo wa fedha kiasi cha Sh 100,000 ni Erasmus Barongo wa Iringa Tanzania, Wilfred Magige wa Magomeni, Dar es Salaam, Ramadhan Juma wa Tanga Makorora, Ulusura Mohamed wa Kihonda Morogoro na Fredy Wandola wa Uyole Mbeya.
Katika Promosheni hiyo, msomaji wa Mwanaspoti anachotakiwa kufanya ni kununua gazeti hili ambapo ukurasa wa pili atakuta kuponi anayotakiwa ijazwe kwa kuweka taarifa sahihi kisha atume kipande alichojaza kwenda ofisi za gazeti hili  zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam  au aikabidhi kwa wauza magazeti waliopo jirani naye.
Msomaji anashauriwa kucheza mara nyingi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kushinda.

Advertisement