Azam yamchelewesha Ndayiragije Stars

Friday July 12 2019

 

By Charles Abel

KAIMU Kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amepanga kuanika mikakati yake kwa timu hiyo mara baada ya mchezo wa Azam na Bandari FC ambao ni wa Kombe la Kagame leo Ijumaa.
Ndayiragije ameteuliwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuisimamia kwa muda Stars, kufuatia kutimuliwa kwa kocha Emannuel Amunike hivi karibuni.
Amunike alitimuliwa baada ya Stars kufanya vibaya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Misri.
Ndayiragije amesema akili yake kwa sasa ni kuhakikisha Azam inaibuka na ushindi dhidi ya Bandari FC na baada ya hapo atazungumzia uteuzi wake Stars.
"Nashukuru kupata nafasi hiyo lakini kwa sasa siko katika nafasi nzuri kulizungumzia hilo. Nadhani baada ya mchezo wa kesho (leo) nitakuwa kwenye nafasi ya kulijadili hilo," alisema Ndayiragije.
Jana Alhamisi, TFF, ilimteua kocha huyo wa zamani wa klabu za Vital'O, Mbao FC na KMC, kuwa kocha wa muda wa Stars kwa ajili ya kuiandaa timu hiyo kuelekea mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Mbali na Ndayiragije, Juma Mgunda wa Coastal Union na Seleman Matola wa Polisi Tanzania waliteuliwa kama makocha wasaidizi wa kikosi hicho sambamba na Saleh Ahmed Machupa ambaye atahudumu nafasi ya ukocha wa makipa.
Nahodha wa zamani wa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' yeye ameteuliwa kuwa Meneja wa timu hiyo akichukua nafasi ya Danny Msangi.

Advertisement