Aussems ageuka ‘mbogo’ kwa nyota wake Simba

Muktasari:

Wachezaji wa Simba ambao watakosekana mechi ya Ngao ya Jamii kutokana na kusumbuliwa kwao na majeruhi ni Aishi Manula, Ibrahim Ajibu na mshambuliaji wa Kibrazil, Wilker Henrique da Silva.

Dar es Salaam. Simba inajiwinda kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi UD Songo ya Msumbiji, lakini Kocha Patrick Aussems amesema hatampanga mchezaji kutokana na ukubwa wa jina lake.

Timu hizo zinarudiana Agosti 23 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Maputo, Msumbiji Jumamosi iliyopita.

Akizungumza wakati wa mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, jijini, Aussems alisema ameridhishwa na mapokeo ya wachezaji wake katika mafunzo yake, lakini amewataka kuongeza juhudi ili kupata namba kikosi cha kwanza.

“Kwa ujumla naridhishwa na maandalizi yetu, lakini siwezi kusema nani nitampa nafasi ya kucheza katika mchezo huo, kila mchezaji anatakiwa kutunza nidhamu ndani na nje ya uwanja.

“Mchezaji atakayenishawishi katika mazoezi ndiye nitampa nafasi ya kucheza. Unauliza kama nina ‘first eleven’, hapana, mimi natoa nafasi kwa kila mmoja ambaye atatimiza wajibu wake vizuri katika mafunzo,” alisema Aussems.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema ana kikosi kipana baada ya kufanya usajili aliodai umekidhi viwango alivyokuwa akitaka kwa ajili ya ushindani katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Aussems alisema ripoti yake ilifanyiwa kazi kwa kuongeza wachezaji wapya ambao anaamini wataongeza nguvu hasa katika safu ya ulinzi ingawa kazi kubwa anataka kuelekeza katika kuimarisha eneo la kiungo na ushambuliaji.

Alisema ujio wa Haruna Shamte na Gadiel utaongeza nguvu katika eneo la pembeni alilodai msimu uliopita lilikuwa na changamoto baada ya kukosekana Shimari Kapombe aliyekuwa majeruhi.

"Nataka tuendelee kucheza kuanzia nyuma, ni muhimu kuwa bora na imara eneo hilo kabla ya kwenda mbele,  upana wa kikosi unatoa wigo wa kuwa na machaguo mengi.

"Msimu uliopita tulipambana na nawajibika kama kocha kukiimarisha kikosi changu ili kuwa bora kwenye eneo hilo japo pia nafanyia kazi maeneo mengine, " alisema kocha huyo.

Aussems alisema anafanyia kazi eneo la kiungo na ushambuliaji ili kuendelea kuwa bora katika maeneo hayo Simba imeondokewa na James Kotei aliyetimkia, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Emmanuel Okwi aliyejiunga na Al Ittihad ya Misri.

Wanaopewa nafasi kuvaa viatu vya nyota hao ni Sharaf Eldin Shiboub ambaye ameonekana akicheza kwenye eneo la Kotei kwenye michezo iliyopita ya Simba na Deo Kanda ambaye alionyesha uwezo wake dhidi ya Power Dynamos.

“Wanaweza kufanya vizuri   zaidi ni suala la muda tu kwao, siwezi kuficha juu ya michango ya Kotei na Okwi waliitendea haki jezi za Simba kila mmoja wetu tuliwafurahia, lakini ni lazima maisha mengine yaendelee,” alisema.

Akiuzungumzia mchezo wa Jumamosi ambao watacheza dhidi ya Azam kwenye mchezo wa ufunguzi wa msimu, Aussems alisema kutwaa ngao ya hisani itakuwa  ishara njema kwao msimu.

Wachezaji wa Simba ambao watakosekana mechi ya Ngao ya Jamii kutokana na kusumbuliwa kwao na majeruhi ni Aishi Manula, Ibrahim Ajibu na mshambuliaji wa Kibrazil, Wilker Henrique da Silva.