KMC, Yanga kimewaka

Mwanza. Licha ya KMC kutangulia kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa winga wake machachari, Hassan Kabunda, lakini Yanga ilirejea kwa kasi na kuweza kusawazisha na kufanya timu hizo kwenda mapumziko kwa nguvu sawa.

Katika mchezo huo ambao unapigwa Uwanja wa CCM Kirumba, kila timu ilicheza kwa umakini lakini KMC ikionekana kushambulia zaidi na pasi zao kufika eneo husika licha ya Kipa Mnata kufanya kazi ya ziada.

Kabunda aliiandikia bao la kwanza KMC akiwachambua vyema mabeki kisha kumtazama Mnata na kuachia shuti lililoenda hadi wavuni na kuwafanya mashabiki wa Yanga kupoa kwa muda.

Yanga waliendeleza mashambulizi ya hapa na pale ambapo dakika ya dakika ya 39 Beki wa KMC, Vincent Andrew alimvuta straika wa Yanga, Michael Sarpong na kuoneshwa kadi ya njano na kusababisha penalti iliyozaa bao kwa kufungwa na Tuisila Kisinda.

Pamoja na kwenda mapumziko kwa nguvu sawa, ilionekana KMC kuwa na mipango mizuri lakini ikiponzwa na rafu za mara kwa mara na kusababisha faulo nyingi ambazo Yanga kama wangezitumia vizuri wangeweza kuongoza kipindi cha kwanza.

KMC itajilaumu kwa nafasi kadhaa ilizopata bila mafanikio kuanzia dakika ya nane kupitia David Bryson na dakika ya 16 kupitia kwa Kenny Ally ambazo hatari zao zilitoka nje na moja kuokolewa na Mnata.

Yanga wao walikosa mabao kupitia kwa Wazir Junior ambaye alishindwa kuunganisha vyema mpira wa kona uliopigwa na Kisinda dakika ya 27 na Sarpong dakika ya 33 aliposhindwa kuumiliki vyema mpira wa faulo wa Deus Kaseke.