Wanne wamtia njaa Manula

ACHANA na vita ya wafungaji mabao katika Ligi Kuu Bara, kama hujui kuna ligi ndogo ya makipa ambapo wanne wameanza kumtia njaa Kipa Bora kwa misimu mitatu mfululizo, Aishi Manula wa Simba.

Aishi ameidakia Simba mechi tano msimu huu na kuruhusu mabao katika michezo miwili dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar, kwa maana ya kuwa na ‘clean sheet’ tatu, akiachwa mbali na Danile Mgore wa Biashara United, David Kissu wa Azam, Metacha Mnata wa Yanga na Abdultwalib Mshery wa Mtibwa Sugar.

Kissu na Mgore ndio wakali kwa kucheza mechi tano bila kuruhusu nyavu kuguswa, wakifuatiwa na Metacha na Mshery wenye ‘clean sheet’ nne kila moja.

Ikumbukwe msimu uliopita katika tuzo za Ligi Kuu Bara, Mgore aliingia kwenye kinyang’anyiro iliyokwenda kwa Manula ambaye kwa sasa ni wazi atakuwa na kazi kubwa ya kutaka kulinda heshima yake mbele ya makipa hao anaochuana nao.

Kocha wa zamani wa makipa Yanga, Juma Pondamali alizungumzia ushindani huo kwa kusema ligi msimu huu ni ngumu kutokana na timu nne kuwa zinashuka moja kwa moja na nyingine mbili zinakwenda kucheza hatua ya mtoano - kwa maana hiyo makipa watakuwa na kazi kubwa ya kufanya.

“Tutaona timu nyingi zitakuwa zikicheza kwa kushambulia, sasa hapa ndio tutaona kazi ya makipa yule ambaye atakuwa bora ndiye ataweza kumaliza mechi nyingi bila kufungwa,” alisema Pondamali.