Ulinzi mazoezi Yanga usipime

INAPOFIKA mechi ya Simba na Yanga bwana kazi huwa ni kubwa kweli kweli

Wachezaji wanakuwa katika presha, makocha na hata mashabiki wote wanakuwa tofauti na mechi nyingine.

Hicho ndicho kimetokea hata katika mazoezi ya Yanga yanayofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Cha Sheria maeneo ya Mawasiliano Ubungo baada ya kuwekwa ulinzi mkali.

Katika kuonyesha kuwa wanadhibiti hujuma uongozi wa Yanga umeweka doria kwenye mazoezi hayo kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kuingia kutazama.

Si waandishi wa habari, mashabiki wala viongozi wasio na  vitambulisho maalum wanaoruhusiwa kuingia kutazama mazoezi hayo.

MCL Digital ilifika uwanjani hapo saa 10 : 30 jioni na mlinzi kufungua geti kisha kuonyesha ishara ya kutaka magari yote kupaki pembeni.

Mlinzi huyo akisimamisha magari anamuita mmoja wa makomandoo waliokuwa karibu na geti hilo ambao ndio wanaruhusiwa kumuhoji mtu yoyote anayeingia hapo ambaye sio mwanachuo.

"Hapa haruhusiwi mtu yoyote kwenda kutazama mazoezi,hii ni amri kutoka kwa kocha na viongozi wa juu.

"Yaani hata kiongozi yeyote akija hapa kama hana hii beji (anaonyesha beji aliyovaa shingoni) haruhusiwi kuingia.

"Yaani tumekatazwa kabisa, hakuna anayeruhusiwa kuingia katika kambi ya Yanga iwe mazoezini au kambini mpaka hiyo mechi ipite"amesena komandoo huyo.

Anaongeza" Yaani hii mechi ipite tu maana hata sisi tunachoka kukesha kulinda timu, ninavyokwambia hapa leo siku ya nne sijalala nyumbani ili kuifanya kazi hii ya ulinzi".