Simba hakuna kulala yaanza kujifua mapema kuikabili Azam

Muktasari:

Simba ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 12 baada ya kushinda mechi zao nne za ligi

Dar es Salaam. Simba imeendelea kujifua kwenye Uwanja wa Uhuru kujiandaa na mechi yake dhidi ya Azam FC itakayopigwa Oktoba 23, 2019.

Simba ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wameshinda mechi zao nne za ligi hiyo hivyo mchezo dhidi ya Azam ni kipimo kwao kizuri kuelekea katika kutimiza ndoto yao ya kutetea ubingwa wao.

Katika mazoezi hayo nahodha John Bocco ameshindwa kufanya na wenzake kutokana na kuendelea kuuguza majeraha yake.

Wachezaji waliofanya mazoezi hayo ni Makipa Aishi Manula na Beno Kakolanya, Said Ndemla, Meddie Kagere, Wilker Da Silva, Tairone, Da Santos, Fraga, Hassan Dilunga.

Wengine  Pascal Wawa, Shiboub, Shomary Kapombe, Ibrahim Ajibu, Deo Kanda, Haruna Shamte, Kennedy Juma na Yusuph Mlipili.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema mazoezi hayo yakuwaandaa kuwa fiti na wana mpango wa kucheza mechi ya kirafiki.

"Hatutakuwa na mapumziko ya kupisha timu ya Taifa, tunataka wachezaji wawe fiti, pia tutaangalia kama tutacheza mechi ya kirafiki."

"Kwa sababu kikosi kipo pungufu kutokana na wengine kuwa kwenye majukumu ya Taifa Stars, tukitaka kucheza mechi basi tunaweza kuchukua wa kikosi B."

"Tunaamini waliopo Stars wanafanya mazoezi ya kuwa fiti ndio maana hata hawa tumeamua kuwafanyisha mazoezi ili watakapoungana na wenzao kikosi kiwe kwenye kiwango sawa," alisema Rweyemamu.