Tanzania yapanda nafasi mbili viwango FIFA

Thursday September 19 2019

Tanzania yapanda, Mwanaspoti, Michezo,  nafasi mbili, viwango FIFA

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Tanzania imepanda kwa nafasi mbili kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mwezi Septemba.
Katika viwango vilivyotangazwa leo na FIFA, Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 137 hadi nafasi ya 135.
Kupanda huko kunaonekana kumechagizwa na timu ya Taifa 'Taifa Stars' kufanya vizuri kwa kufuzu hatua ya makundi ya kuwania kutinga Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 zitakazofanyika Qatar.
Stars iliitupa nje Burundi kwenye hatua ya awali kwa ushindi wa mikwaju ya penati 3-0 baada ya timu hizo kutoka sare ya jumla ya mabao 2-2 kwa mechi mbili zilizokutanisha timu hizo nyumbani na ugenini ambapo kila mchezo matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1.
Rwanda imepanda kwa nafasi tatu kutoka ile ya 133 hadi ya 130, Kenya imebakia kwenye nafasi yake ya 107, Burundi imepanda kwa nafasi nne kutoka ile ya 148 hadi ile ya 144 wakati Uganda imebakia katika nafasi ya 80 ambayo ilikuwepo pindi viwango hivyo vilipotangazwa mwezi uliopita.

Advertisement