Goodluck Gozbert Staa wa injili anayeumizwa na mapenzi

Muktasari:

Zamani ndio nilikuwa naumizwa sana na coment kwenye mitandao ya kijamii lakini siku hizi nimezoea na huwa wakati mwingine  napotezea au nasoma coment nabaki tu nacheka.

DAR ES SALAAM. “Kwa ibada nasinzia sijui mdudu kaingia ee ila nikiona bia nasikia kuchangamkaa..niko na ubaya.. niko na ubaya... niko na ubaya, Bwana (Mungu) nibadilishe.”
Ni moja ya wimbo wa dini unaotikisa kwa sasa Tanzania na hata nje ya Tanzania, kwenye mitandao ya kijamii watu wakiuimba kwa fujo hasa vijana.
Katika jamii ya leo, vijana wengi wa sasa ni wagumu sana kupenda nyimbo za dini, lakini ukiona mpaka wimbo wameukubali basi ujue umewagusa.
Vijana wengi wameupenda sana wimbo huu ambao umeimbwa na mwimbaji Goodluck Gozbert na kitu kikubwa ambacho wamekipenda sana ndani ya wimbo huo ni jinsi alivyoimba katika mahadhi ya kizazi kipya (Bongo Fleva)
Katika video ya wimbo huo, msanii huyo pamoja na wacheza shoo wake wameuongezea mvuto wimbo kwa kucheza staili mbalimbali ambazo wakati mwingine hutumika katika nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva na dansi, jambo ambalo limezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii. ....Katika video ya wimbo huo, msanii huyo pamoja na wacheza shoo wake wameuongezea mvuto wimbo kwa kucheza staili mbalimbali ambazo wakati mwingine hutumika katika nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva na dansi jambo ambalo limezua mjadala  kwenye mitandao ya kijamii.
“Nashukuru Mungu wimbo  wa Nibadilishe umekuwa na mapokeo makubwa  na kutengeneza historia katika maisha yangu ya muziki.
“Tangu nianze kufanya muziki wa dini, sijawahi kuwa na wimbo uliotrendi  kwa kiasi kikubwa kama huu na hii inaonyesha watu wameupokea  na ujumbe umefika,” anasema Goodluck.
Goodluck anasema licha ya nyimbo zake nyingi zinapendwa na watu wa rika zote lakini huu wa Nibadilishe umeonekana kupokewa zaidi na vijana na kuamini lengo lake limefanikiwa.
“Lengo langu huduma yangu iwafikie watu wengi zaidi lakini hasa vijana ili waache njia mbaya na kumgeukia Mungu na ndiyo maana umeona hata katika wimbo huu nimejaribu  kuutengeneza ili kuwavutia vijana wengi  na kwa jinsi walivyoupokea naamini meseji imeenda na imepokelewa.
“Ndiyo maana unaona baadhi ya watu wanahoji  kwa nini labda mmecheza vile au umeimba kwa staili hiyo na kuona kama nimepotoka lakini hawajui hakuna jambo zuri kama kuangalia watu wanataka nini kwa wakati huo na ufanye nini ili kuwabadilisha watu kwa haraka wamjue Mungu kupitia uimbaji.
Anasema wimbo huo ametumia gharama kubwa kutengeneza ingawa hawezi kuzitaja lakini anashukuru Mungu kuna baadhi ya watu walimsaidia  ili kukamilisha kurekodi video hiyo.
“Huwa siendagi bar wala kwenye kumbi za starehe (club) lakini ilinibidi kufanya hivyo ili kuhakikisha ujumbe unafika kwa jamii kwa kuhakikisha nafanya kitu ili kuonyeha uhalisia,” anasema Goodluck
Hata hivyo, licha ya baadhi ya watu kudai msanii huyo kaimba na kucheza kibongofleva sana katika wimbo huo lakini yeye  anaona kawaida tu na wala haoni maneno ya watu kama changamoto kwake.
“Zamani ndio nilikuwa naumizwa sana na coment kwenye mitandao ya kijamii lakini siku hizi nimezoea na huwa wakati mwingine  napotezea au nasoma coment nabaki tu nacheka.
“Nilipotoa wimbo wa Ipo Siku, Acha waambiane, unakuta kwenye mtandao wa kijamii mtu anaibuka na kukwambia wewe ni shetani na mfuasi wa kuzimu.
Nikawa najiuliza nimemkosea nini Mungu nikaishia kuvumilia na mwisho nikazoea kwani naamini wakati mwingine changamoto zinapokukabili zinakujenga na kukuimarisha zaidi,” anasema Goodluck.

Vipi kuhusu mwonekano wake
Mwimbaji huyo licha ya kuimba kama msanii wa Bongo Fleva  lakini hata mwonekana wake kimavazi unashabihiana kwa kiasi kikubwa na wasanii wa nyimbo hizo za kizazi kipya. 
“Huwa nakutana nalo sana hilo suala la watu kuhoji mwonekana wangu na wengine kusema haipaswi mtumishi kuvaa hivyo au kunyoa nywele hivyo, lakini lazima wajue wale ambao Mungu amekusudia niwape huduma wananielewa sana na wale wananiangalia juu juu watabaki  kunijaji lakini  hilo jambo sijaliweka kama changamoto kwangu.
Anasema nguo zake ananunua popote tu hata akipita Karume akiiona nguo ya mtumba nzuri  anaagizwa iletwe ili mradi tu impendeze.
“Nguo yoyote  hata kama 1000 ilimradi ni nzuri na imenitosha nanunua ingawa naweza nikafika hadi Karume lakini kushuka kwenye gari sitashuka nitaagiza mtu tu kwa sababu wakati mwingine ukishuka unaweza kuleta msongamano kwa sababu kila mtu atataka akusalimie.
“Siwezi kudharau nguo za mtumba kwa sababu nimefanya hiyo biashara wakati nikiwa Mwanza, kwani  maisha yetu hayakuwa mazuri na ukizingatia tulibaki na mama tu, hivyo ilikuwa lazima tupambane kuhakikisha tunaishi vizuri,” anasema

Anawakwepa  totoz balaa
Goodluck amekiri anatongozwa sana na wasichana lakini hana muda nao kwani anasubiri wakati sahihi wa Mungu atakayempatia mke mwema.
“Kama kutongozwa natongozwa sana tu, kuanzia kwenye mitandao ya kijamii, kanisani na wengine wananiambia live lakini nawapotezea kwani bado wakati wangu wa kuoa.
“Sina ndoa, sina mchumba na wala sitafuti kwa sasa. Kuna wakati ilikuwa inatokea hiyo fursa najikuta najaribu  kuwa na msichana lakini nashindwa. Yaani anatokea msichana unamwelewa na yeye anakuelewa inafika muda mfupi mnashindwana basi mnaachana.
“Mfano mnapendana na msichana lakini kumbe anakuja kwako akitaka vitu fulani labda uwe unamtoa sehemu mbalimbali za starehe lakini anakukuta wewe umebobea kwenye maombi  anakuacha anakwambia endelea na Mungu wako. Hali hiyo ilivyozidi nikaona bora nitulie nisubiri wakati  sahihi wa Mungu ambao naamini atanipatia mke mwema wa kufanana naye,” anasema na kuongeza siku akioa idadi ya watoto itatagemea na hali ya kipato chao kwa kipindi hicho.

Amewahi kuumizwa katika mapenzi
Goodluck anakwambia kupenda kusikie tu  kwani yakikukuta  unaweza ukaona dunia chungu.
“Nimeshawahi kuumizwa sana kwenye mapenzi. Nakumbuka wakati huo sina jina kubwa niliwahi kumpenda dada mmoja sitamtaja jina lakini alichonifanyia  eee!” anasema Goodluck huku akionekana kubadilika sura  
Anaendelea, ”Baadae akaniacha na sijui sababu mpaka leo.Iliniumiza sana yaani we fikiria mtu unampenda  halafu hakutaki tena  na kila siku unapita mbele ya nyumba yao hayo maumivu yake unayopata huwezi kuelezea na ilinichukua muda mrefu kumsahau.Sijui yuko wapi kwa sasa kwani hajawahi kunitafuta na wala mimi sina mpango wa kumtafuta,” anasema Goodluck.

Rais Magufuli alimletea Nongwa
Goodluck anasema hatasahau siku aliyoalikwa na Rais John Pombe Magufuli Ikulu kwenda kutumbuiza kwani imebaki kuwa kumbukumbu muhimu katika maisha yake.
“Kualikwa na Rais Ikulu ni jambo kubwa sana na litabaki kumbukumbu moyoni mwangu.
“Ingawa ile siku iliniletea shida kwani tangu kipindi kile nilivyotoka pale watu waliamini sasa mimi ni tajiri. Yaani nilipewa heshima ya kualikwa Ikulu lakini heshima hiyo ilikuja na majukumu. Unakuta mtu anakwambia naomba kiasi fulani cha pesa, ukimwambia sina  anasema  haiwezekani umekutana na Rais ukose hela hiyo,” anasema Goodluck.

Kumbe anaangalia sana Bongo Fleva
Goodluck anasema  huwa anaangalia  sana tu muziki wa Bongo Fleva na haoni kama ni dhambi kwani hata wanamuziki wanaoimba muziki huo wanaimba kwa ajili ya kuburudisha.
“Huwa naangalia sana muziki wa Bongo fleva na sioni kama kuna tatizo  ili mradi muziki huo hauvunji maadili.
Hata hivyo, Goodluck alikataa kata kata  kutaja msanii gani wa Bongo Fleva anayemkubali huku akisema kuwa kama wao haajawahi kukiri hadharani  wasanii gani wa injili wanaowakubali basi yeye hata siku moja hatasema anayemkubali.

Humwambii kitu kwa wali maharage
Mwanamuziki huyo anasema Wali Maharage ndio chakula namba moja anachokipenda huku pia akipenda sana ugali na dagaa.
“Yaani ninyime vyote sio wali maharage na wakati mwingine huwa napika mwenyewe nyumbani kwani  nakaa na mdogo wangu na tukiwepo nyumbani tunapeana zamu  ya kupika.”

Akiri muziki unalipa.
Goodluck anasema licha ya kwamba anafanya muziki kama huduma lakini inalipa kwa kiasi chake kwani huwa wanalipwa kupitia mtandao wa You Tube ingawa huwa hapendezwi na wanaosema kuwa anafanya muziki kama biashara .
“Unapoweka wimbo yotube kila mwezi unalipwa  kutokana na idadi ya watazamaji wanaotazama nyimbo yako”.
Lakini hiyo haimaanishi kuwa tunafanya muziki wa dini kama biashara.Wakumbuke  kuwa tunaimba kwa ajili ya watu,Mungu alichokiweka ndani yetu ndicho tunawapatia wao na ili kiwafikie kwa wingi zaidi ndio maana tunaweka katika mitandano kama You tube,” anasema Goodluck.

Msanii wa Injili anayemkubali
Mwanamuziki huyo anasema wasanii wenzake wote wa injili anawaopenda  na kusikiliza nyimbo zao lakini anamkubali zaidi Angel Benard kwani ana sauti ya kipekee.
Pia, Goodluck amesema anamkubali pia Rose Muhando na anamuombea kwa Mungu amalize changamoto zote anazopitia na arejee lwa nguvu katika huduma yake ya uimbaji.

Wimbo wake Bora.
Goodluck ana nyimbo kali  zinazobamba kama Ipo Siku, Acha waambiane, Hao hao, Nipe, Hauwezi kushindana, Nipe na Nibadilishe lakini hakuna wimbo anaoukubalu kama Shukrani.
“Yaani katika nyimbo zangu zote,Shukrani ni wimbo bora kwangu wa muda wote. Ni wimbo ambao  kila siku unanifanya nimshukuru Mungu.Huo wimbo umeeleza kila  kitu kuhusu maisha yangu,” anasema.