Ashley Cole astaafu, kurudi kivingine

Tuesday August 20 2019

Ashley Cole astaafu, kurudi kivingine, Mwanaspoti, Michezo, Mwanasport

 

LONDON, ENGLAND. KILA chenye mwanzo kina mwisho. Beki wa kushoto matata kabisa, Ashley Cole ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 38 huku akitamba kwenye soka la kibabe kwa miaka 20.
Staa huyo wa zamani wa Arsenal, Chelsea na timu ya taifa ya England ametangaza kustaafu juzi Jumapili na hivyo kudai kwamba sasa anafikiria kuhamishia mipango yake ya kimaisha kwenye mambo mengine ikiwamo ukocha.
Beki, Cole ni moja kati ya wachezaji tisa walioichezea England mara 100, huku kukiwa na wachezaji watano tu ndio wanaozidi baada ya yeye kucheza mechi 107. Baada ya kuibukia akitokea kwenye kikosi cha watoto wa Arsenal, Cole alihamia Chelsea kwa utata mwaka 2006 kabla ya kwenda AS Roma, LA Galaxy na hatimaye kwenye kumalizia maisha yake ya soka Derby msimu uliopita.
Akicheza chini ya aliyekuwa mchezaji mwenzake Frank Lampard, Derby ilicheza mechi ya mchujo wa kuwania kupanda Ligi Kuu England, lakini walichapwa na Aston Villa uwanjani Wembley. Na sasa Cole anataka kuhamia kwenye ukocha tayari ameshaanza kozi mbalimbali.
"Baada ya kufikiria kwa kina sasa, nimeona sasa ni wakati mwafaka kutundika daruga," alisema.
"Sasa natazama mambo mengine na bila shaka nitaingia kwenye ukocha. Nachukua kozi ya ukocha kwa sasa, nataka niwe kocha bora kabisa duniani."
Cole amecheza mechi 697 kwenye ngazi ya klabu katika maisha yake ya soka, akishinda mataji 13 yakiwamo matatu ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja. Kombe la FA ameshinda mara saba, Europa League mara moja na ameingia mara mbili kwenye kikosi bora cha mwaka cha Uefa.

Advertisement